Wanaswa wakisafirisha dhahabu Mbeya

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na kikosi kazi cha madini cha taifa linawashikilia watuhumiwa 10 wakazi wa Ilomba jijini Mbeya kwa tuhuma za kusafirisha na kutorosha vipande vya madini ya dhahabu.
Taarifa iliyotolewa leo Machi 19, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga imeeleza kuwa watuhumiwa walikamatwa Machi 16, 2024 maeneo ya Veta Ikulu wakiwa na vipande 314 vya dhahabu vyenye uzito wa gramu 9,622.76 yenye thamani zaidi ya Sh bilioni 1 bila kuwa na kibali.

Katika taarifa yake, Kuzaga amesema watuhumiwa walikutwa na vifaa vingine ambavyo ni vipimo vya dhahabu, majiko, mitungi ya gesi na kasiki ya kuhifadhi fedha.
Amesema kuwa watuhumiwa wamekuwa wakitorosha madini hayo kupitia njia zisizo rasmi kwa lengo la kukwepa kulipia kodi, ushuru na gharama nyingine zinazohitaji kwa wafanyabiashara ya madini.




