TOSCI yatoa somo uhakiki wa mbegu bora

MWANZA: WAKULIMA kutoka Kanda ya Ziwa na mikoa jirani wamehimizwa kujifunza mbinu mpya za kidijitali kugundua mbegu feki na halisi za mazao kupitia Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yanayoendelea viwanja vya Nyamongolo jijini Mwanza.
Akizungumza Agosti 3, 2026, Meneja wa Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Kanda ya Ziwa, Ayubu Mushema, amesema maonesho hayo yanalenga kutoa ujuzi mpya kwa wakulima kukabiliana na janga la mbegu feki ambazo zimekuwa zikichangia upatikanaji wa mavuno hafifu.
Amesema wakulima watapata ujuzi wa kidigitali na utambuzi kwa sababu katika mizunguko ya sasa kumekuwa na wimbi kubwa la udanganyifu hasa katika maswala ya mbegu za mazao hivyo wakulima watakuwa na elimu ya kutosha ya utambuzi.

“Mara nyingi mbegu bora ni zilizofanyiwa mchakato wa utafiti na ugunduzi, uhakiki bora wa mbegu katika masoko ya hapa umekuwa ukifanywa na taasisi yetu na mpaka sasa tumerahisisha mfumo wa kugundua mbengu bora zinazofaa kwa kilimo hasa kwa kuficha namba za siri ambazo mteja akiingiza bure kwenye simu yake ya mkononi atapata majibu,” amesema.
Maonesho hayo yamefunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye aliwataka wananchi wa mikoa ya Mwanza na Geita na mikoa jirani kutumia vyema maonesho hayo.


