Sekta binafsi kupewa nafasi kubwa Dira 2050

ARUSHA: WAZIRI Mkuu amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji mabadiliko ya mtazamo kuhusu sekta binafsi, akisisitiza kuwa sekta hiyo imepewa nafasi ya kutekeleza asilimia 70 ya dira hiyo ili kusaidia Serikali kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana na umaskini.

Amesema mitazamo ya kuiona sekta ya umma kuwa ndiyo pekee inayoweza kufanya shughuli za maendeleo kwa uzalendo, huku uwekezaji wa sekta binafsi ukitazamwa kwa mashaka, inaweza kudhoofisha utekelezaji wa Dira 2050 na hatimaye kuathiri maendeleo ya nchi.

Waziri Mkuu amesema hayo leo wakati akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la Wanamipango, akiwataka wanamipango kuwa chachu ya kubadilisha mitazamo hiyo na kuhakikisha mipango ya taifa inatekelezwa kwa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Amesema katika utekelezaji wa Dira 2050, Tanzania haiwezi kufikia malengo ya kupunguza umaskini na kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana bila kuwa na sekta binafsi imara inayoshiriki kikamilifu katika uwekezaji, uzalishaji na uundaji wa ajira.

“Tumeliweka Dira kwamba itatekelezwa kwa asilimia 70 na sekta binafsi. Kama mambo yote yatafanywa na sekta ya umma, hapo siyo uzalendo. Mawazo ya aina hii hayafelishi tu sekta binafsi, bali yanaifelisha dira yote na tutakuwa tunaifelisha nchi,” amesema.

Alisema Tanzania bado ina kazi kubwa ya kuondokana na mtazamo uliodumu kwa muda mrefu wa kuamini kuwa Serikali ndiyo inapaswa kuendesha kila shughuli za kiuchumi, akisema hali hiyo ni sehemu ya changamoto inayopaswa kushughulikiwa katika utekelezaji wa Dira 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button