MaadhimishoTosamaganga kukusanya Sh bilioni 1

IRINGA: Shule ya Sekondari Tosamaganga imezindua kampeni ya kukusanya Sh bilioni moja kwa ajili ya kuboresha miundombinu yake na kununua basi jipya la wanafunzi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 1926.
Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Benjamin Sitta, ukiashiria mwanzo wa kampeni itakayowaunganisha wahitimu wa zamani (Alumni), taasisi, kampuni binafsi na wadau wengine wa maendeleo katika kuwekeza kwenye mustakabali wa shule hiyo, ambayo imekuwa miongoni mwa taasisi zenye historia ndefu zaidi ya elimu nchini.
Sitta alisema Jubilee ya miaka 100 haitakuwa sherehe ya kukumbuka historia pekee, bali itakuwa jukwaa la kuanzisha miradi ya maendeleo itakayoendelea kunufaisha vizazi vijavyo shuleni hapo.
“Tunazindua rasmi maandalizi ya Jubilee ya Miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosamaganga, taasisi iliyoanzishwa mwaka 1926 na ambayo kwa kipindi cha karne moja imeendelea kuwa nguzo ya elimu bora, maadili na uongozi nchini Tanzania,” alisema.
Maadhimisho hayo yatafanyika chini ya kauli mbiu “Miaka 100 ya Elimu Bora, Maadili na Uongozi wa Kuigwa,” ambayo, kwa mujibu wa Sitta, inaakisi mchango wa shule hiyo katika kuzalisha viongozi, wataalamu na watumishi waliochangia maendeleo ya taifa kwa miongo mingi.

Kamati ya Jubilee imeeleza kuwa fedha zitakazopatikana kupitia kampeni hiyo zitatumika kukarabati majengo yaliyochakaa, kuboresha mabweni, kununua samani za wanafunzi, kupata basi jipya pamoja na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo kulingana na mahitaji ya shule.
Ratiba ya maadhimisho inaanza Oktoba 8 kwa matembezi ya Jubilee na shughuli za usafi wa mazingira, zikifuatiwa na mbio za Fun Run Oktoba 9 zitakazowakutanisha Alumni, wanafunzi na wananchi.
Kilele cha maadhimisho kitafanyika Oktoba 10 kwa maonesho ya historia ya shule, nyaraka na kumbukumbu zake, utoaji wa tuzo za heshima pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wa zamani, Edward Nzalalila, aliyesoma Tosamaganga kati ya mwaka 1968 na 1971, alisema Jubilee hiyo ni fursa ya kurejesha shukrani kwa taasisi iliyowajenga viongozi na wataalamu wengi.
“Ni tukio la kihistoria. Tushirikiane kutoa msaada wa hali na mali ili shule hii iendelee kulea viongozi na wataalamu kwa miaka 100 mingine ijayo,” alisema.

Nzalalila alisema sehemu ya miundombinu ya shule imechakaa kutokana na umri wake, hivyo ushiriki wa wahitimu na wadau utasaidia kuiwezesha Tosamaganga kuendelea kutoa elimu bora kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sasa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Alumni, Iddy Mwerangi, alisema kamati imeamua kuwapa wadau uhuru wa kuchagua miradi wanayotaka kuifadhili, kuanzia ukarabati wa mabweni na maabara hadi ununuzi wa samani na maboresho mengine ya shule.
“Kama mtu ana uwezo wa kukarabati bweni lote, anakaribishwa. Kama anaweza kujenga maabara ya kisasa, anakaribishwa. Kama anaweza kununua basi, anakaribishwa,” alisema.
Alisema Alumni tayari wamechukua jukumu la kuhakikisha shule inapata basi jipya la wanafunzi lenye thamani ya takribani Sh Milioni 150, ambalo litakuwa sehemu ya urithi wa maadhimisho ya miaka 100.
“Tunataka basi litakalobeba historia ya miaka 100 ya Tosamaganga. Hili ni jukumu ambalo sisi kama Alumni tumeamua kulisimamia kwa nguvu zetu zote,” alisema.

Waandaaji wanatarajia Jubilee hiyo kuwakutanisha maelfu ya wahitimu wa zamani kutoka ndani na nje ya Tanzania, viongozi wa serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo katika maadhimisho yatakayoadhimisha karne moja ya shule hiyo na kuweka msingi wa maendeleo ya miaka 100 ijayo.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1926 chini ya Misheni ya Kanisa Katoliki kabla ya baadaye kuingia chini ya usimamizi wa serikali, Tosamaganga imeendelea kujijengea sifa ya kuwa miongoni mwa shule zilizozalisha viongozi, wataalamu na watumishi waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania.


