Victoria Group Fun Run kufanyika Agosti 8

BAADA ya zaidi ya miaka 26 ya kujenga urafiki, kusaidiana na kuwekeza pamoja, Victoria Group (VG) sasa imehamishia nguvu zake kwenye mapambano ya kuboresha afya za wanachama wake na jamii kupitia mazoezi ya mwili, ikizindua mbio maalumu za VG Fun Run zitakazofanyika Agosti 8, 2026 katika Victoria Park, Ununio jijini Dar es Salaam.
Waandaaji wa tukio hilo wanasema hatua hiyo imechochewa na ukweli kwamba wanachama wengi wa kundi hilo sasa wamevuka umri wa miaka 50, hali inayowalazimu kuweka afya mbele ili kuendelea kufurahia maisha na shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya VG Fun Run, Isidori Msaki, alisema kundi hilo limeona ni wakati muafaka kuhamasisha utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, si kwa wanachama pekee bali pia kwa wananchi wengine.
Alisema Victoria Group ina wanachama 113 ambao pamoja na familia zao wanafikia takribani watu 700, hivyo wameamua kutumia tukio hilo kama jukwaa la kuhamasisha maisha yenye afya na kuimarisha mshikamano.
Kwa mujibu wa Msaki, mbio hizo za kilomita 10 zitaanza saa 12:00 asubuhi, huku kila mshiriki atakayemaliza akitunukiwa medali na kupata huduma ya supu, wakati wadhamini wa tukio watapewa vyeti vya shukrani kwa mchango wao.
Alifafanua kuwa tukio hilo limefunguliwa kwa wananchi wote, marafiki na wadau mbalimbali, ambapo washiriki wasiokuwa wanachama wa Victoria Group watalipa Sh30,000 zitakazowezesha kupata fulana maalumu, namba ya ushiriki na medali baada ya kumaliza mbio.
Kwa wale wasioweza kukimbia kilomita 10, alisema waandaaji wameandaa mazoezi ya aerobics yatakayoendeshwa na wakufunzi wa mazoezi, sambamba na burudani ya muziki na shughuli nyingine za kijamii zitakazofanyika Victoria Park.
Msaki alisema hadi sasa zaidi ya washiriki 126 wamejisajili, huku lengo likiwa kufikisha zaidi ya washiriki 200 kabla ya siku ya tukio.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Victoria Group, Sabasaba Mushingi, alisema kikundi hicho kilianzishwa miaka 26 iliyopita kwa lengo la kuunganisha marafiki katika kusaidiana nyakati za furaha na huzuni, lakini kadri miaka ilivyosonga wamepanua shughuli zao hadi kwenye uwekezaji wa kiuchumi.
Alisema kwa sasa Victoria Group inamiliki vitega uchumi mbalimbali, ikiwemo Victoria Park inayokadiriwa kuwa na thamani inayozidi Sh bilioni moja, pamoja na uwekezaji katika hati fungani za Serikali na hisa.
Mushingi alisema VG Fun Run ni mwanzo wa mpango wa muda mrefu wa kuifanya kuwa mbio za kila mwaka zitakazovutia washiriki wengi zaidi kutoka ndani na nje ya kundi hilo.
Aliongeza kuwa baada ya tathmini ya tukio la mwaka huu, uongozi unapanga kuliboresha kwa kuongeza zawadi, kupanua ushiriki na kulitumia kama jukwaa la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi Agosti 8 kushiriki siku ya mazoezi, afya na burudani, akisisitiza kuwa afya bora ndiyo msingi wa jamii yenye nguvu na maendeleo endelevu.



