KKKT yatoa mwongozo wa kiroho, kimaandalizi kukabiliana na El Niño

ARUSHA: Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na mamlaka nyingine za Serikali zikiendelea kutoa tahadhari kuhusu msimu ujao wa mvua za vuli unaotarajiwa kunyesha kati ya Oktoba na Desemba 2026 na kuambatana na hali ya El Niño katika maeneo mbalimbali nchini, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limewataka waumini wake kuchukua hatua nane ili kuepuka athari zinazotarajiwa.

Katika waraka uliotolewa na Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Dk Alex Malasusa, wenye kichwa cha habari “Angalizo la Kiroho na Kimaandalizi Kuhusu Mvua za Vuli na Hali ya El Niño katika Nchi Yetu,” na kusomwa katika makanisa ya dhehebu hilo nchini leo, KKKT limetaka maandalizi yafanywe kuhusu namna ya kukabiliana na tishio la mafuriko ili kupunguza athari endapo yatatokea.

Kanisa hilo limesisitiza kuwa limelichukulia kwa uzito mkubwa tishio la El Niño na kuwataka waumini wake kuchukua tahadhari, likibainisha kuwa majanga na maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kusababisha mateso makubwa duniani kote.

Kwa msingi huo, Kanisa limewataka washarika wote wa KKKT kuzingatia yafuatayo:

1. Maombi

Kanisa limewataka waumini wake kutokata tamaa katika kufanya maombi, likisisitiza: “Mungu wetu ni Mungu anayesikia. Pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, anaweza kutenda zaidi ya tunavyowaza—hivyo tusichoke kumwomba atuepushe na maafa.”

2. Maombi maalumu

Kanisa limewataka washarika wote kufanya maombi maalumu katika ibada za Jumapili tatu zifuatazo: Septemba 20, Septemba 27 na Oktoba 4, 2026, kama ifuatavyo:

a) Jumapili, Septemba 20, 2026: Kuombea familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na mafuriko nchini Nepal, pamoja na kuiombea Serikali ya Nepal ipewe hekima, busara na rasilimali za kuwahudumia wananchi wake.

(Wachaguliwe wanaume wawili na wanawake wawili miongoni mwa washarika waaminifu kuongoza zamu za maombi.)

b) Jumapili, Septemba 27, 2026: Kuomba toba kwa ajili ya Tanzania na kumsihi Mungu kuilinda nchi dhidi ya tishio la El Niño ambalo linaweza kusababisha mafuriko; kuiombea Serikali ipewe hekima, maarifa na rasilimali za kukabiliana na majanga; na kuliombea Kanisa na jamii kwa ujumla kupewa uwezo na maarifa ya kujiandaa na kukabiliana na majanga.

(Wachaguliwe wanaume wawili na wanawake wawili miongoni mwa washarika waaminifu kuongoza zamu za maombi.)

c) Jumapili, Oktoba 4, 2026: Itakuwa Jumapili ya mwisho ya maombi hayo, ikiwa ni siku ya kumshukuru Mungu.

“Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.” — Zaburi 136:1

B. Maandalizi ya kukabiliana na El Niño endapo itatokea

3. Kila muumini na kila jumuiya wahimizwe kufuatilia taarifa rasmi za TMA kuhusu mwenendo wa hali ya hewa na kuchukua tahadhari mapema badala ya kusubiri hadi mafuriko yatokee.

4. Kama hatua ya awali, KKKT imeandaa vipeperushi vya uhamasishaji kuhusu El Niño kwa ajili ya kufikisha ujumbe huo kwa wanajamii, makanisa yote na vituo vya Kanisa, ili wafuatilie kwa karibu taarifa kuhusu tishio hilo na kuendelea kuhamasisha jamii kujiandaa kukabiliana nalo.

5. Dayosisi na vituo vya Kanisa viweke utaratibu na kutenga rasilimali za kuwezesha kukabiliana na El Niño, ikiwa ni pamoja na kusafisha mifereji ya maji na miundombinu ya maji.

6. Kila jumuiya ihakikishe kuwa maeneo ya ibada na makazi ya waumini yana mifumo salama ya kupitisha maji ya mvua ili kupunguza uharibifu endapo kutakuwa na mvua kubwa.

7. Kupitia ibada za jumuiya, zitambuliwe familia zinazoishi katika maeneo hatarishi na zichukuliwe hatua za tahadhari kwa kuandaa mipango ya kuzilinda endapo El Niño itatokea, ili kuzuia madhara makubwa.

8. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania litaendelea kuwasiliana na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na wadau mbalimbali. Pia litashirikiana na mtandao wa viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali katika kufanya maandalizi ya kukabiliana na janga la El Niño endapo litatokea, kwa lengo la kuhakikisha usalama wa jamii ya Watanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button