Tume ya Madini yaimarisha ukaguzi migodi

DODOMA: Tume ya Madini imeendelea kuimarisha ukaguzi wa migodi ili kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia sheria, usalama wa wafanyakazi, afya kazini na utunzaji wa mazingira, hatua inayolenga kujenga sekta ya madini yenye tija na endelevu.
Akizungumza jijini Dodoma, Mjiolojia na Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Paschal Juma, amesema Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira chini ya Mkurugenzi wake, Mhandisi Hamisi Kamando, ina jukumu la kusimamia na kufuatilia shughuli zote za uchimbaji ili kuhakikisha zinazingatia Sheria ya Madini, kanuni, sera na miongozo mbalimbali ya sekta hiyo.

Amesema Kurugenzi hiyo hufanya ukaguzi wa usalama na afya mahali pa kazi, hufuatilia utekelezaji wa mipango ya usimamizi wa mazingira, urejeshaji wa maeneo yaliyochimbwa pamoja na mipango ya ufungaji migodi kwa kuzingatia viwango vinavyolinda mazingira na kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, amesema Kurugenzi hiyo hupitia na kuidhinisha mipango ya uchimbaji, taarifa za utendaji wa migodi na usanifu wa miundombinu ya migodi, huku ikisimamia matumizi salama ya baruti kwa mujibu wa Sheria ya Baruti, Sura ya 45, na kanuni zake.

Paschal amesema Tume ya Madini inatumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kutoa elimu kwa wananchi, wachimbaji na wadau wa sekta kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga, mbinu salama za uchimbaji, utunzaji wa mazingira pamoja na uhifadhi na matumizi salama ya baruti.

Amesisitiza kuwa elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wadau, kuimarisha uzingatiaji wa sheria na viwango vya usalama, kupunguza ajali migodini na kuendeleza sekta ya madini inayochangia ukuaji wa uchumi wa taifa kwa njia endelevu.



