VG Marathon 2027 kupigwa kilometa 21

DAR ES SALAAM: Mbio za VG Fun Run 2026 zimefanyika kwa shamrashamra na mwitikio mkubwa wa washiriki, huku mamia ya wakimbiaji na wapenzi wa mazoezi wakijitokeza kushiriki mbio hizo za kilomita 5 na 10 zilizoanzia Ununio hadi Zahanati ya JKT Mbweni jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo zilizofanyika leo, Agosti 8, zimeweka msingi wa hatua kubwa zaidi mwaka 2027, baada ya Victoria Group (VG) kutangaza mpango wa kuziendeleza kuwa nusu marathon ya kilomita 21.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya VG Fun Run, Isidori Msaki, alisema mafanikio na mwitikio wa mbio za mwaka huu vimewapa hamasa ya kuongeza umbali huo mwakani.
Alisema maandalizi yataanza mapema, huku akiwataka washiriki kuendelea na mazoezi ili kujiandaa na changamoto ya mbio hizo mpya.

Naye Mwenyekiti wa Victoria Group, Sabasaba Mushingi, alisema mafanikio ya VG Fun Run yamevuka hatua ya kuwa tukio la kudumu litakalofanyika kila mwaka Agosti 8.
“Kuanzia mwakani tutakuwa na VG Fun Run kila tarehe 8 mwezi wa nane ili tuweze kupata fursa ya kukutana na kubadilishana mawazo na kujenga afya zetu,” alisema.

Mushingi aliipongeza kamati ya maandalizi kwa kufanikisha mbio hizo, huku akiwashukuru wadhamini mbalimbali, Jeshi la Polisi na watoa huduma za afya kwa kuhakikisha usalama wa washiriki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ukopeshaji CRDB, Musa Lwila, alisema CRDB Foundation itaendelea kuunga mkono VG Fun Run, akisisitiza umuhimu wa jamii kuwekeza katika afya kupitia mazoezi.

Lwila, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CRDB Fitness Club, alisema anatarajia mwaka 2027 kuwaleta wanachama wa klabu hiyo kushiriki mbio hizo ili kuongeza hamasa na ushindani.



