Sh Milioni 120 zatengwa zawadi CRDB Marathon

DAR ES SALAAM: BENKI ya CRDB imetenga zaidi ya Sh milioni 120 kwa washindi wa mbio za marathon zitakazofanyika Agosti 16 Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
Zawadi kwa atakayetwaa medali ya dhahabu kwa mbio za kilometa 42 atazawadiwa Sh milioni 12, huku washindi wengine wa pili mpaka sita nao wakitarajiwa kuondoka na fedha kwa viwango tofauti.
Kwa upande wa mbio za Kilometa 21, atakayetwaa medali ya dhahabu ataondoka na Sh milioni sita na pia kutakuwa na mbio za baiskeli za Kilometa 65 zenye zawadi nono.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB benki Foundation, Tully Mwambapa amesema lengo la mbio hizo ni kuhamasisha Watanzania kufanya mazoezi, kujenga afya ya mwili na akili, pamoja na kuwaunganisha watu kupitia michezo na burudani.
“Maandalizi ya mbio hizi yamefikia hatua kubwa na asilimia 89 ya lengo la ushiriki likiwa tayari limefikiwa. Tunaendelea kuwahimiza watu kujitokeza kwa wingi kwani tutakuwa na washiriki kutoka ukanda wa Afrika Mashariki,”amesema na kuongeza:
“Tumetenga zawadi za zaidi ya Sh milioni 120. Hakuna mdau mwingine Tanzania ambaye amewahi kutenga kiwango hicho kikubwa cha fedha .”
Mbio hizo zitahusisha pia kilometa 5, 10 kwa wakimbiaji na watembeaji, huku CRDB ikisema njia zote zimefanyiwa majaribio na kuthibitishwa kwa kushirikiana na kampuni za kimataifa zenye utaalamu wa kusimamia mazingira ya marathon.
Kwa mujibu wa Mwambapa, mbio hizo zimeendelea kupata mwitikio kutoka ndani na nje ya Tanzania, ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi, ambako shughuli zinazohusiana na marathon zimefanyika.



