Walimu wajengewa uwezo teknolojia kufundishia

KILIMANJARO; Walimu 215 kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kilimanjaro wamepatiwa mafunzo yanayolenga kuongeza uwezo wao wa kutumia teknolojia na rasilimali za kidijitali katika ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo katika Ukumbi wa SMMUCo, Ofisa Elimu Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Ntupwa, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha walimu kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya elimu na kutumia rasilimali zilizopo kuboresha ufundishaji.

Alisema walimu wanapaswa kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia katika kazi zao za kila siku, ili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na nyenzo mbalimbali za kujifunzia kwa urahisi.

“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea walimu uwezo wa kutumia rasilimali rahisi za kidijitali, ikiwemo kuunda na kutumia makundi ya WhatsApp, kutafuta vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwenye mtandao, kushirikishana nyenzo za masomo na kuwaelekeza wanafunzi namna ya kutafuta taarifa na nyenzo mbalimbali za kielimu mtandaoni,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa SMMUCo, Prof Andrew Mmbwambo, alisema ushirikiano wa taasisi mbalimbali za elimu umechangia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa mpango huo na kuhakikisha walimu wanapata ujuzi unaohitajika katika mazingira ya sasa ya ufundishaji.

Prof Mmbwambo alisema mpango huo pia unalenga kuimarisha matumizi ya rasilimali za kidijitali shuleni, hususan katika maeneo yenye upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Alisema mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali, zikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nelson Mandela African Institution of Science and Technology, Mwalimu Nyerere Memorial Academy, VETA na taasisi ya elimu ya walimu kutoka Uswisi, pamoja na taasisi nyingine.

“Ushirikiano huu umedumu kwa takribani miaka tisa, tangu mwaka 2014, ukiendelea kutoa mafunzo kwa walimu kila mwaka. Hili linatupa faraja sana kwani walimu mbalimbali wamepata ujuzi na wanaupeleka kwa wanafunzi,” alisema.

Amesema mafunzo hayo yanafanyika kwa makundi mawili, ambapo kundi moja hupatiwa mafunzo kwa wiki moja na kundi jingine hufuata katika wiki inayofuata na kwamba walimu 215 kutoka shule mbalimbali katika wilaya zote za Kilimanjaro wanatarajiwa kunufaika.

Mafanikio ya mpango huo yanaonekana kupitia ushuhuda wa mwalimu Jeniffer Laurence ambae ni mnufaika wa mafunzo hayo,ambaye alieleza kuwa ameweza kuunda kundi la WhatsApp kwa ajili ya wazazi wa wanafunzi, kupitia ambalo hushirikisha maelekezo, notes na taarifa mbalimbali zinazohusiana na masomo.

Hivyo, WhatsApp imekuwa zaidi ya chombo cha mawasiliano na sasa inatumika kusaidia ufundishaji na mawasiliano kati ya walimu, wanafunzi na wazazi.

Mwalimu mwingine, Holiness John , alieleza namna mafunzo hayo yalivyomsaidia kuhusisha wanafunzi katika shughuli za vitendo zinazohusiana na ubunifu na utengenezaji wa bidhaa za nguo.

Kupitia shughuli hizo, shule imeweza kushirikisha wataalamu kama washonaji na mafundi, huku baadhi ya bidhaa zikitengenezwa kwa ajili ya matumizi au kuuzwa nje ya mazingira ya shule.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button