Aliyedaiwa kufagia fedha na nywele saluni adakwa
GEITA; Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia Faustine Zakaria, ambaye ni kinyozi kwa tuhuma za kuharibu kwa makusudi fedha halali za Tanzania kinyume na sheria za nchini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Safia Jongo, ametoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa Faustine alionekana akitenda kosa hilo kupitia picha mjongeo.
Amesema picha mjongeo zilimuonesha Faustine akifagia noti alizokuwa amezitawanya sakafuni, zikiwa zimechangamana na nywele zilizotokana na shughuli za unyoaji na uchafu mwingine ndani ya saluni yake.
“Picha mjongeo hiyo mtuhumiwa alirekodiwa kwa ridhaa yake huku akifahamu wazi kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria.
“Baada ya kurekodi aliisambaza picha hizo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii Agosti 23, 2026, hatua iliyowezesha mamlaka za kisheria kufuatilia tukio hilo na kuchukua hatua stahiki,” imeelezwa.
Amesema Jeshi la Polisi linakamilisha uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika.



