Twende Butiama sasa ni Nyerere Cycling Tour

DAR ES SALAAM: Msafara wa baiskeli wa Twende Butiama umepewa jina jipya la Nyerere Cycling Tour, katika hatua inayolenga kuenzi urithi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, huku mchezo wa baiskeli nchini ukifunguliwa ukurasa mpya wa ushindani wa kimataifa.
Mabadiliko hayo yametangazwa na Kampuni ya Vodacom kwa kushirikiana na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA), sambamba na uzinduzi wa mashindano mapya ya Vodacom Coastal Classic, mbio za kilomita 109 zinazolenga kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya mchezo wa baiskeli.
Kwa mujibu wa waandaaji, jina jipya la Nyerere Cycling Tour linaakisi dhamira ya msafara huo ya kuenzi maono ya Mwalimu Nyerere kuhusu heshima, usawa na fursa kwa kila Mtanzania, huku likilenga pia kuupa msafara huo nafasi ya kukua na kuwa jukwaa la mashindano ya kiwango cha kimataifa.

Wadau na washiriki wa msafara wa mbio za Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) wakipiga makofi kama ishara ya kufurahia ujio wa mashindano ya mbio za Vodacom Coastal Classic.
Msafara huo, ulioanzishwa mwaka 2016, umejikita katika kuunganisha mchezo wa baiskeli na juhudi za kuboresha fursa za elimu kwa watoto nchini.
Hadi sasa, zaidi ya shule 107 zimefikiwa kupitia mpango huo, huku zaidi ya wanafunzi 75,000 wakinufaika na maboresho ya mazingira ya kujifunzia, ikiwamo ujenzi wa madarasa bora na jumuishi, miundombinu ya vyoo pamoja na vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Vodacom Tanzania Foundation ilianza kushirikiana na CHABATA kufadhili msafara huo miaka minne iliyopita. Katika kipindi hicho, msafara huo umekua kwa kiasi kikubwa na kuvutia washiriki kutoka Tanzania, nchi za Afrika Mashariki na mataifa mengine duniani.

Mwanzilishi wa Msafara wa Mbio za Twende Butiama, Gabriel Landa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimu mpya wa msafara wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) utakaozinduliwa mnamo mwezi wa kumi.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema kampuni hiyo inalenga kutumia mashindano hayo kuhamasisha Watanzania wengi zaidi kuingia katika mchezo wa baiskeli na kuwapa nafasi ya kuendeleza vipaji vyao.
Alisema waendesha baiskeli wengi wanaonekana kila siku kwenye barabara za Tanzania, lakini wanahitaji vifaa na mafunzo sahihi ili waweze kushindana katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Tunataka kukuza mchezo huu. Hakuna sababu kwa nini Abella kutoka Mwanza asiweze kushindana hapa Tanzania na kwenye majukwaa ya kimataifa, au Saidi kutoka Shinyanga. Wanachohitaji ni vifaa sahihi na mafunzo sahihi,” alisema.

Wadau wa msafara wa Cycling tour (zamani Twende Butiama) wakisikiliza kwa makini kuhusu msimu mpya wa msafara huo na ujio wa Mashindano ya Vodacom Coastal Classic utakaozinduliwa mnamo mwezi wa kumi mwaka huu.
Kwa upande wake, mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa, alisema msafara huo umevuka mipaka ya kuwa safari ya baiskeli na sasa umejikita katika kuendeleza maono ya Mwalimu Nyerere kuhusu heshima na fursa sawa kwa Watanzania.
Alisema kubadilishwa kwa jina la msafara huo, sambamba na kuanzishwa kwa Vodacom Coastal Classic, ni mwanzo wa safari mpya inayolenga kujenga jukwaa la kuibua vipaji vya ndani na kuvutia waendesha baiskeli kutoka sehemu mbalimbali duniani.



