Sh Bil 11 kukamilisha ujenzi kituo cha saratani Mbeya

MBEYA; Serikali imewekeza takribani Sh bilioni 11 katika ujenzi wa Kituo cha Saratani cha Ocean Road (ORCI) Mbeya, kinacholenga kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani karibu na wananchi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Diwani Msemo, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza mzigo kwa wagonjwa wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam kupata huduma za kibingwa na kibobezi za saratani.

Amesema ujenzi wa vituo vya kikanda ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kupanua huduma za saratani nchini na kuongeza upatikanaji wa huduma katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dk Msemo, kituo hicho kina umuhimu wa kimkakati kutokana na nafasi ya Mbeya kama lango la Tanzania kuelekea Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Amesema kituo hicho kitakapokamilika kitatoa fursa kwa wagonjwa kutoka Tanzania na nchi jirani kupata huduma za saratani katika ukanda huo, jambo litakaloweza pia kuchochea utalii wa tiba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea, amesema Serikali inaendelea kupanua huduma za saratani na kujenga vituo vya kikanda ili kuongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza safari ndefu kwa wagonjwa.

Amesema takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kuwa takribani watu milioni 20 duniani waligundulika kuwa na saratani, huku milioni 9.7 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Kwa Tanzania, amesema wagonjwa wapya wa saratani wanakadiriwa kufikia takribani 45,000 kwa mwaka, huku karibu 30,000 wakipoteza maisha.

Dk Nyembea amesema takribani asilimia 50 ya saratani zinaweza kuzuilika, huku nyingine zikiwa na uwezekano wa kugundulika mapema na kutibiwa.

Amesema serikali inapanga kujenga vituo vingine vya saratani katika maeneo ya Arusha, Kigoma na Mtwara.

Mkandarasi wa mradi huo, Ally Mtigita, amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika Januari 2027.

Amesema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 57 na mradi huo una thamani ya takribani Sh bilioni 10.4.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button