Vyombo vya usafiri vyajipanga AFCON 2027

DAR ES SALAAM: Kampuni ya Azam Marine imeanza maandalizi ya kuhakikisha inatoa huduma bora za usafiri wa majini kuelekea michuano ya AFCON 2027.

Kampuni hiyo imeongeza meli mpya ya Kilimanjaro 9 iliyowasili Januari mwaka huu ambapo hatua hiyo inalenga kuimarisha usafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar kwa mashabiki, wachezaji na viongozi pamoja na abiria wengine watakaohitaji kutumia usafiri wa majini wakati wa michuano hiyo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Marine, Abubakari Aziz Salim, amesema kampuni hiyo imefanya maandalizi mbalimbali kuelekea mashindano hayo, huku akieleza kuwa ongezeko la meli hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uwezo na ufanisi wa huduma kwa abiria.

Amesema Azam Marine ina uwezo wa kusafirisha hadi abiria 15,000 kwa siku kati ya Dar es Salaam na Zanzibar na kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam, idadi ambayo ni sawa na uwezo wa uwanja wa Amani kuhudumia watu kwa wakati mmoja.

Amesisitiza kuwa Azam Marine ina uzoefu wa miaka 33 katika sekta ya usafiri wa majini, hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kuhudumia ongezeko la wasafiri linalotarajiwa wakati wa AFCON 2027, na kuongeza kuwa maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha mashabiki na wadau wa michuano wanapata usafiri salama na wenye ufanisi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button