Wanafunzi 1,700 Bagaza wafaidika msaada wa mahindi, sukari

GEITA: TAASISI ya Mapung’o Foundation imetoa msaada wa magunia 30 ya mahindi na kilo 250 za sukari kwa Shule ya Msingi Bagaza iliyopo Kata ya Butobela wilayani Geita.

Msaada huo unalenga kusaidia upatikanaji wa uji shuleni hapo kwa wanafunzi zaidi ya 1,700 na kuwatengenezea mazingira bora ya kujifunzia ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua kiwango cha elimu na ufaulu.
Mratibu wa Mapung’o Foundation, Marco Victor amekabidhi msaada huo kwa niaba ya taasisi na kueleza kuwa taasisi hiyo imejizatiti kusaidia mahitaji ya wanafunzi kwa manufaa ya jamii.

Ofisa Elimu wa Kata ya Butobela, John Otieno amekiri kuwa msaada huo utasaidia kuinua kiwango cha elimu na kuleta ahueni ya michango ya chakula kwa wazazi.
Otieno amewaomba wadau wengine kuiga mfano wa Mapung’o Foundation kwa kujitolea kuchangia vyakula mashuleni, akieleza kuwa hatua hiyo inaimarisha afya na maendeleo ya elimu kwa watoto.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bagaza, Damasi Madata, amesema shule hiyo hutumia debe tatu za mahindi kwa siku kwa ajili ya uji hivo magunia 30 ya mahindi pamoja na kilo 250 za sukari vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha programu ya lishe shuleni.



