Stamico yawekeza Sh milioni 40 mkaa mbadala Geita

GEITA: SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limetoa ufadhili wa jumla ya Sh milioni 40 kwa wazalishaji wa mkaa mbadala mkoani Geita ambao ni Taasisi ya Wanawake na Samia ili kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia mkoani Geita, Adelina Kabakama ametoa taarifa hiyo mbele ya viongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa Mwaka 2026.

Kabakama amesema kupitia mradi huo Taasisi ya Wanawake na Samia Geita itashirikiana na STAMICO kuunga mkono jitihada za kuzalisha na kuuza mkaa wa nishati safi.

Amesema hatua hiyo inalenga kutekeleza mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa mwaka 2024/34 kwa kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wanatumia Nishati safi ifikapo 2034.

“Mradi huu unanufaisha wananchi kwani gharama za mkaa huu ni nafuu, pia mkaa huu ni nishati rafiki kwa mazingira kwani hupunguza matumizi ya kuni na kupunguza ukataji wa miti ili kutengeneza mikaa.

“Kwa sasa tunasambaza wastani wa tani 03 kwa mwezi, na tumenuwia kupeleka kwenye taasisi mbalimbali za umma na kulingana na ongezeko la mahitaji”, amesema Kabakama.

Amesema ili kukidhi mahitaji, STAMICO imepanga kujenga kiwanda cha mkaa mbadala mkoani Geita ili kusogeza huduma kwa wateja na kuendelea kuweka ukaribu kwa watanzania kupata nishati safi kwa ukaribu”, amesema.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa kwa Mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’oda amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia inapaswa kuungwa mkono na kila mtu kwani inalenga kuimarisha usalama wa afya za binadamu na mazingira.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button