Twikondele yafikisha mizinga 117 ya kisasa

SHINYANGA: KIKUNDI cha Ufugaji Nyuki Twikondele kilichopo katika kijiji cha Buyange, Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala, kimefanikiwa kuongeza mizinga ya nyuki ya kisasa hadi kufikia 117 baada ya kupata ufadhili kutoka Kampuni ya Mgodi wa Barrick Bulyanhulu.

Kikundi hicho kimeeleza kuwa ufadhili huo, uliokwenda sambamba na mafunzo na fursa za kutembelea maonyesho mbalimbali ya biashara, umewawezesha kuboresha ufugaji nyuki na kujifunza namna ya kutafuta masoko ya bidhaa zao.

Katibu wa kikundi hicho, Daniel Nkwande, amesema hayo leo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, alipofika katika eneo la mradi wa ufugaji nyuki na kitalu cha miti ya matunda, mradi uliogharimu Sh milioni 25.

Nkwande amesema kabla ya kufikia hatua ya kuwa na mizinga 117 ya kisasa, kikundi hicho kilianza shughuli za ufugaji nyuki mwaka 2015 kikiwa na mizinga saba ya kawaida.

Amesema Barrick Bulyanhulu pia imewapatia mafunzo mbalimbali, kuwawezesha kushiriki maonyesho ya biashara na kuwajengea uwezo wa kutafuta masoko, huku wakihamasishwa kupanda miti ya matunda kama sehemu ya uhifadhi wa mazingira.

“Kabla ya kufikia hatua ya kuwa na mizinga 117, tulianza ufugaji mwaka 2015 tukiwa na mizinga saba ya kawaida tuliyokuwa tukiifuga kwenye kikundi chetu,” amesema Nkwande.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Semkondo, amesema kampuni hiyo awali ilikifadhili kikundi hicho kwa mizinga saba kama hatua ya majaribio, na baada ya kuona kinafanya vizuri ikaongeza ufadhili kwa kuwapatia mizinga 110 ya kisasa.

Semkondo amesema kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na jamii inayozunguka mgodi kwa kuwawezesha kupitia mafunzo, vifaa na fursa za kujifunza katika maonyesho ya biashara.

Amesema ufugaji nyuki umeanza kuleta manufaa kwa wanakikundi, wakiwemo kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kutekeleza shughuli nyingine za maendeleo.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amepongeza kikundi hicho kwa kuunganisha ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira kupitia uoteshaji wa vitalu vya miti ya matunda.

Mwang’onda amewataka kuendelea kutunza mazingira na kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za uhifadhi, akieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara wa utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ninawapongeza kikundi hiki kwa uhifadhi na kuotesha vitalu vya miti ya matunda. Kila mmoja awe rafiki wa kuhifadhi mazingira,” amesema Mwang’onda.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button