Bosi NIMR asifu umuhimu wa tiba asili mfumo huduma za afya

MBEYA; MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof Said Aboud, amesema asilimia 60 hadi 70 ya Watanzania huanza kutafuta matibabu ya tiba asili kabla ya kufika hospitalini, hali inayoonesha umuhimu wa tiba hiyo katika mfumo wa huduma za afya nchini.
Prof Aboud amesema kutokana na hali hiyo, NIMR inatoa huduma jumuishi katika hospitali za rufaa za mikoa 14 nchini, zinazompa mgonjwa fursa ya kuchagua kati ya tiba asili na huduma za hospitali, kwa lengo la kupanua wigo wa huduma za afya.

Amesema hayo leo wakati wa Kongamano la Tano la Kisayansi la Tiba Asili lililofanyika jijini Mbeya ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika, ambapo wataalamu wanawasilisha matokeo mbalimbali ya tafiti kuhusu tiba asili.
Amesema hadi sasa kuna takribani dawa 45 za tiba asili zilizosajiliwa katika mfumo, huku NIMR ikiwa imehusika katika dawa 11,kupitia kituo cha utafiti Mabibo, Dar es Salaam, kinachojihusisha na utafiti na uzalishaji wa dawa za tiba asili.
“Jukumu la NIMR ni kufanya utafiti ili kuangalia usalama, ufanisi na ubora wa dawa za tiba asili ambazo zimetengenezwa na NIMR, watafiti wetu au wataalamu wa tiba asili,” amesema Prof Aboud.

Amewataka wananchi kutumia dawa za tiba asili zilizohakikiwa na kuthibitishwa usalama, ufanisi na ubora wake, akisisitiza kuwa matumizi holela yanaweza kusababisha madhara.
Ameongeza kuwa Serikali imewekeza katika ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji wa dawa za tiba asili katika Kituo cha Utafiti cha NIMR Mabibo, Dar es Salaam, ambacho kinatarajiwa kufunguliwa katika Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Prof Nicolao Otieno, amesema hadi sasa dawa 200 zimesajiliwa, huku zaidi ya 40 kati yake zikiwa zimepelekwa katika huduma jumuishi.

Amesema Mamlaka hiyo imeanza kufanya msako ili kubaini dawa zote zilizoingia nchini bila kufuata sheria na taratibu zilizowekwa huku akionya kuwa dawa ambayo haijasajiliwa hairuhusiwi kuingia sokoni wala kutumika nchini..
Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI), Balozi Dk Mpoki Ulisubisya, amesema Serikali haiwezi kuruhusu matumizi ya tiba asili zisizothibitishwa ambazo zinaweza kuhatarisha afya za wananchi.
Amewataka wataalamu kuongeza kasi ya tafiti na ugunduzi katika eneo la tiba asili ili kuwezesha wananchi kupata huduma na dawa salama, zenye ufanisi na ubora unaokubalika.



