Mtaalamu: Elimu zaidi inahitajika uelewa tiba asili

MBEYA; Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya Wizara ya Afya, DK Winfrida Kidima,amesema jamii bado ina uelewa tofauti kuhusu tiba asili, hivyo Wizara ya Afya inaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa huduma hizo, hasa katika kuboresha afya ya wananchi.
Dk Kidima amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya.
Amesema tiba asili, ni maarifa ya ndani yaliyorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na ambayo yamekuwa yakitumika katika kutibu na kutatua changamoto mbalimbali za afya, lakini baadhi ya Watanzania wanahusisha tiba hizo na imani za kishirikina.

“Wizara ya Afya imejikita zaidi katika kuangalia huduma zinazohusiana na dawa, lakini kwa sasa tuko kwenye mchakato wa kuangalia zile tiba na mbinu ambazo zinaweza kusaidia katika matibabu,” amesema Dk Kidima.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa tiba hizo hatua iliyowezesha kuanzisha huduma jumuishi za tiba za asili na zile zinazotolewa hospitali kwa kuzingatia miongozo ya huduma za afya.
Ameeleza kuwa ujumuishaji wa tiba asili katika mfumo wa afya unaendelea hatua kwa hatua, huku Serikali ikiendelea kujifunza na kufanya maboresho kulingana na miongozo iliyowekwa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema, amesema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa wa jamii na kuhamasisha wataalamu wa tiba asili, watafiti, wasimamizi, wataalamu wa afya, wawekezaji, wazalishaji na wadau wa maendeleo kushiriki katika kuendeleza tiba asili kwa usalama na uendelevu.

Dk Nyema amewataka wananchi na wadau mbalimbali kushiriki katika shughuli zitakazofanyika katika kipindi chote cha maadhimisho hayo akisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mchango wa tiba asili katika huduma za afya unaendelezwa kupitia utafiti wa kisayansi, udhibiti, uhakiki wa ubora na ujumuishaji unaofaa katika mfumo wa afya.
Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika Kitaifa yaliyoanza Agosti 25,2026,na kilele chake kitakachofanyika Agosti 31, 2026 yakiongozwa na kaulimbiu: “Juhudi katika Utafiti wa Tiba Asili kuelekea Huduma za Afya kwa Wote.”



