Wazee wapamba mapokezi ya mwenge Missenyi

KAGERA: Wazee wa kimila maarufu kama Abenkorogo katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera wamepamba mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwa kujitokeza kwa wingi wakiwa wamevalia mavazi yao ya asili.

Wazee hao walionekana wakiwa wamevalia kanzu nyeupe, koti na kofia, huku wakiwa wameshika fimbo pamoja na kubeba vibuyu mikononi wakati wa kuupokea Mwenge wa Uhuru.

Walishiriki katika mapokezi hayo yaliyofanyika katika Kijiji cha Gera wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali mstaafu Hamis Maiga, na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Siima. Wazee hao pia walipata fursa ya kuushika Mwenge huo.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, amesema amefurahishwa na namna wazee hao wa kimila walivyoshiriki katika tukio hilo muhimu la kushuhudia Tunu ya Taifa.

Mwang’onda amewataka wazee hao kuendelea kuwa mabalozi wa kuhubiri amani na mshikamano kwa vijana wao, huku wakitunza na kuutukuza utamaduni wa Mkoa wa Kagera.

Aidha, amewataka kuendelea kudumisha mila na tamaduni zao, kuzihifadhi na kuzisemea kwa vizazi vijavyo ili vijana waweze kujifunza na kukua katika misingi ya maadili mema, amani na mshikamano katika masuala ya kitaifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button