Wananchi Byeju watakiwa kulinda vyanzo vya maji

KAGERA: Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 zimewataka wananchi wa Byeju, Kata ya Mtukula, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, kuepuka shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, kufyeka misitu na ujenzi karibu na vyanzo vya maji kutokana na madhara yanayoweza kujitokeza.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, ametoa kauli hiyo wakati akizindua Mradi wa Maji Byeju wenye thamani ya Sh bilioni 2.4.

Mwang’onda amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilima karibu na eneo la mradi huo wa maji, hali ambayo inaweza kuchochea uharibifu wa mazingira na kuhatarisha uendelevu wa mradi.

Amesema angependa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu upandaji wa miti rafiki kwa vyanzo vya maji, badala ya wananchi kuendelea na shughuli za kilimo na ujenzi katika maeneo ya karibu na vyanzo vya maji.

Aidha, amewapongeza RUWASA kwa kukamilisha mradi huo mkubwa ambao utawanufaisha wananchi wengi wa Kata ya Mtukula.

 

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Missenyi, Roberth Mgombela, amesema mradi huo umekamilika na utaweza kuwahudumia wananchi 26,671.

Amesema tangu kukamilika kwa mradi huo, wananchi 532 tayari wamechangamkia fursa ya kuunganishiwa huduma ya maji majumbani.

Mgombela amesema kwa sasa mradi huo una vituo 16 vya kuchotea maji, matanki ya kuhifadhi maji pamoja na mitambo ya umeme wa jua.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button