Mradi wa ukusanyaji, urejeshaji taka wazinduliwa

DAR ES SALAAM: Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha usafi na utunzaji wa mazingira, Kampuni ya TotalEnergies Tanzania kwa kushirikiana na Arena Recycling Ltd imezindua mradi wa ukusanyaji na urejelezaji wa taka za plastiki jijini Dar es Salaam.

Mradi huo unalenga kupunguza athari za taka za plastiki katika mazingira, huku zikikusanywa na kuongezewa thamani kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo vifaa vya ujenzi kama matofali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Meneja Mauzo wa TotalEnergies Tanzania, Thomas Meitaroni, amesema taka za plastiki ni miongoni mwa taka zinazochukua muda mrefu kuoza na hivyo zinahitaji utaratibu maalumu wa ukusanyaji na urejelezaji.

Amesema kupitia mradi huo, taka hizo zitakusanywa na kuingizwa katika mnyororo wa thamani ili ziweze kutumika kama malighafi na wakati huo huo kutoa fursa kwa Watanzania.

“Tunataka taka hizi zisibaki kuwa changamoto kwa mazingira, bali zigeuzwe kuwa fursa kupitia ukusanyaji na urejelezaji,” amesema.

Meitaroni amesema kwa sasa mradi huo umeanza katika vituo vitano vya mafuta vya TotalEnergies jijini Dar es Salaam, huku kukiwa na mpango wa kuupeleka katika maeneo mengine ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Arena Recycling Ltd, Hellena Sailas, amesema kampuni hiyo inashirikiana katika ukusanyaji na urejelezaji wa taka za plastiki kwa kuzibadilisha kuwa malighafi inayoweza kutumika katika utengenezaji wa vifaa vya ujenzi.

Amesema hatua hiyo inasaidia kupunguza kiasi cha taka kinachoishia katika mazingira, huku ikiwezesha taka hizo kutumika tena katika shughuli za uzalishaji.

Naye Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa TotalEnergies Tanzania, Getrude Mpangile, amesema mradi huo umetokana na wazo la Arena Recycling na umeungwa mkono kwa kuwa unalenga kuchangia usafi wa mazingira na matumizi bora ya taka za plastiki.

Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za wadau mbalimbali kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto ya taka za plastiki na kuendeleza matumizi ya taka kama rasilimali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button