Barabara ya Magereza – Kabalenzi kufungua fursa biashara

KAGERA: Wakazi wa Kata ya Ngara Mjini, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameeleza matumaini makubwa kuwa barabara ya Magereza–Kabalenzi iliyojengwa kwa kiwango cha lami itafungua fursa mpya za biashara, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuongeza kipato cha wananchi.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 0.55 imejengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Wilaya ya Ngara, kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 316, na imezinduliwa katika ziara ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026.

Wananchi wamesema uwepo wa barabara hiyo haujaboreshwa tu mandhari ya mji, bali pia umeondoa changamoto za usafiri na kurahisisha biashara ya mazao na bidhaa mbalimbali, ikiwemo bidhaa zinazosafirishwa kwenda nchi jirani ya Burundi.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Ngara, Mhandisi Mokoro Magori, akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang’onda, amesema ujenzi wa barabara hiyo unalenga kuboresha miundombinu ya usafiri na kubadili sura ya mji.

Amesema barabara hiyo pia itasaidia kupunguza vumbi lililokuwa likiwakabili wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo, huku ikiimarisha mazingira ya kufanya biashara.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang’onda, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa lengo la kuinua hadhi za miji, kupunguza gharama za matengenezo ya barabara na vyombo vya moto, pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Mwang’onda amesema amefurahishwa na utekelezaji wa mradi huo na amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na hadhi za miji ili kuinua uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Wananchi wa mitaa ya Mulugwanza Kati na Ngara Mjini ambako mradi huo unapatikana, akiwemo Benasi Zachali, Dishoni Bwakunga na Manase Ntiluvako, wamemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo, wakisema barabara hiyo imekuwa na thamani kubwa kwao.
Aidha, Mwang’onda amewataka wananchi kuendelea kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kuwanufaisha wananchi.

Barabara ya Magereza–Kabalenzi inatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha shughuli za biashara na usafirishaji katika mji wa Ngara, hususan kutokana na nafasi ya eneo hilo katika biashara zinazovuka mpaka kuelekea Burundi.



