Muleba: Familia mbili zapata mil 4/- za matibabu

KAGERA: Familia mbili wilayani Muleba, mkoani Kagera, ambazo zilikuwa zikikabiliwa na changamoto za matibabu na hali ngumu ya maisha, zimepata msaada wa jumla ya shilingi milioni nne kutoka Taasisi ya Wenfurebe Foundation kupitia Mkurugenzi wake, Simon Patrick Wenfurebe.
Msaada huo umetolewa kwa ajili ya kugharamia matibabu ya wagonjwa katika familia hizo, ambao walikuwa wakishindwa kumudu gharama za matibabu kutokana na hali yao ya kiuchumi.

Kwa baadhi ya familia hizo, changamoto hazikuwa za kiafya pekee, bali pia zilihusisha matatizo ya kifamilia, ikiwemo kutengwa na wenza wao, hali iliyowaweka katika mazingira magumu na kuwafanya kupoteza matumaini ya maisha.

Miongoni mwa walionufaika na msaada huo ni Stewart Onesmo, mkazi wa Muleba, ambaye alikuwa akisumbuliwa na uvimbe kwenye mguu na kuomba msaada wa shilingi laki sita kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Wenfurebe Foundation, Simon Patrick Wenfurebe, alimpatia shilingi milioni moja kwa ajili ya kugharamia upasuaji wa mguu huo.
Mnufaika mwingine ni Anjelina Dauson, mkazi wa Kitongoji cha Kanone, Kijiji cha Kasheno, Kata ya Magata/Karutanga, ambaye mtoto wake anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

Anjelina alikabidhiwa shilingi milioni tatu kwa ajili ya kugharamia upasuaji wa mtoto wake.
Baada ya kupokea msaada huo, familia hizo zimeeleza kuwa zimepata matumaini mapya na kuona mwanga wa kuendelea kupambana na changamoto zinazowakabili.
Mwakilishi wa Wenfurebe Foundation, Suleiman Adam, amesema taasisi hiyo ilipokea taarifa kuhusu hali ya wahitaji hao, na Mkurugenzi wake, Simon Patrick Wenfurebe, akaamua kuingilia kati kwa kutoa fedha za matibabu.
Amesema lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha watu wanaokabiliwa na mazingira magumu hawabaki peke yao, bali wanapata msaada unaoweza kurejesha matumaini na kuwasaidia kuendelea na maisha.

Kwa familia hizo, msaada huo hauonekani tu kama fedha za matibabu, bali pia ni ishara kwamba bado kuna watu na taasisi zinazojali maisha yao na wako tayari kusimama nao wakati wa changamoto.
Wenfurebe Foundation pia imesema imepanga kutenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa mwaka 2026/2027 kwa ajili ya kusaidia familia zenye uhitaji wa matibabu, hususan zile ambazo zimekuwa zikifanya michango ya kusaidia wagonjwa baada ya kupata vibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, mpango huo utakuwa sehemu ya juhudi za kujumuika na jamii ya Wilaya ya Muleba na kusaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto za kiafya na kiuchumi.



