Serikali yasisitiza usahihi wa taarifa

DAR ES SALAAM: Serikali imesisitiza umuhimu wa kusimamia uadilifu, usahihi na ukweli katika mnyororo wa taarifa, hasa katika kipindi hiki ambacho teknolojia ya kidijitali imeongeza kasi ya upatikanaji na usambazaji wa habari.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa (IDUAI), kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari MAELEZO, Evordy Kyando, Mkurugenzi Msaidizi wa Usajili wa Idara hiyo, amesema Serikali inatambua umuhimu wa majukwaa ya wadau wa habari katika kujitathmini na kusikiliza maoni kuhusu utekelezaji wa wajibu wake wa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na zinazoweza kuthibitishwa.

Kyando amesema mazingira ya sasa ya kidijitali yameleta changamoto kutokana na taarifa kusambazwa kwa urahisi na kwa kasi kupitia intaneti, mitandao ya kijamii, simu janja na teknolojia mpya, ikiwemo akili bandia (AI), hali inayoweza kuchangia kuenea kwa taarifa potofu na kuathiri maamuzi ya wananchi.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa taarifa ni haki ya msingi kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Serikali ikiendelea kuweka mifumo na kuboresha sheria zinazoratibu upatikanaji wa taarifa.

Aidha, amesema mapambano dhidi ya taarifa potofu (misinformation) na taarifa zinazotumiwa kwa nia ya kupotosha au kudhuru (malinformation) hayawezi kuachiwa Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa waandishi wa habari na wadau wote wa uhuru wa habari.

Amesisitiza umuhimu wa kila mdau kuhakikisha taarifa zinahakikiwa kabla ya kutumiwa au kusambazwa, huku akieleza kuwa Serikali iko tayari kusikiliza tathmini na kushiriki katika mijadala kuhusu utekelezaji wa sheria za upatikanaji wa taarifa, huduma za vyombo vya habari na sheria nyingine zinazohusiana na sekta hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Mwenyekiti wa Muungano wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI), Ernest Sungura, amesema upatikanaji wa taarifa pekee hautoshi katika zama za kidijitali, bali wananchi wanahitaji taarifa zinazopatikana kwa wakati, zilizo sahihi na zinazoweza kuaminika.

Sungura amesema mazingira ya sasa yamejaa taarifa potofu, taarifa zilizopotoshwa, picha na video zilizohaririwa pamoja na maudhui yanayotengenezwa kwa kutumia akili bandia, hali inayoweza kufanya iwe vigumu kwa wananchi kutofautisha taarifa halisi na bandia.

Amesema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya upatikanaji wa taarifa na uadilifu wa taarifa, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha taarifa zinazotolewa na kusambazwa zinazingatia ukweli na usahihi.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Cash earning job to earns more than $700 per day. getting paid weekly more than $3500 or more simply doing easy work online. no special skills required for this job and regular earning from this are just awesome. all you need is 2 hrs a day for this job and earning are awesome. every person can get this by follow details here…

    THIS→→→→ http://Www.Payathome1.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button