Mchengerwa ataka Afrika ijenge mifumo imara bajeti za afya

Arusha: Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amezitaka nchi za Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani katika sekta ya afya kwa kutenga fedha za kutosha kutoka kwenye bajeti za serikali.
Amesema hatua hiyo itahakikisha huduma za tiba ya dharura zinapatikana wakati wote bila kutegemea misaada ya nje, ambayo imeanza kupungua duniani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Afrika wa Tiba ya Dharura (AfCEM 2026), unaofanyika jijini Arusha kwa siku tatu, Mchengerwa amesema huduma hizo zinapaswa kuwa sehemu ya msingi ya mfumo wa afya, badala ya kutegemea miradi ya ufadhili wa muda maalumu.

Amesema idadi ya idara za tiba ya dharura nchini imeongezeka kutoka saba mwaka 2020 hadi 125 kufikia Machi 2026, ingawa bado kuna changamoto za ajali za barabarani, magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo kiharusi, magonjwa ya moyo, kisukari na figo, pamoja na upungufu wa madaktari bingwa, wauguzi na wahudumu wa huduma za dharura.
–
Amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikadiria kuwa misaada ya nje kwa sekta ya afya ilipungua kwa asilimia 30 hadi 40 mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka 2023, hali iliyosababisha baadhi ya nchi kupunguza huduma na kupoteza watumishi wa afya.
Amesisitiza kuwa changamoto hiyo inapaswa kuwa kichocheo cha Afrika kujenga mifumo imara ya kugharamia huduma zake, akirejea Azimio la Arusha la mwaka 1967 lililosisitiza umuhimu wa kujitegemea katika maendeleo.



