Korosho Queens yalenga fainali wavu Taifa

DAR ES SALAAM: MENEJA wa timu ya wavu ya Korosho Queens ya Mtwara, Hussein Kibombwe amesema timu hiyo imejipanga vizuri katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo baada ya kuanza kwa ushindi katika michezo yake mitatu, huku wakilenga kufika hatua ya fainali.

Akizungumza na DailyNews Digital, Kibombwe amesema tofauti na mzunguko wa kwanza ambao walikabiliwa na changamoto ya upungufu wa baadhi ya wachezaji, kwa sasa kikosi chao kimetimia na wachezaji wote wapo tayari kupambana kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri.

“Tumejipanga vizuri na kikosi chetu kimetimia. Katika mzunguko wa kwanza tulikuwa na changamoto ya upungufu wa wachezaji, lakini sasa tuna wachezaji wote na tumeanza vizuri kwa kupata ushindi katika michezo yetu,” amesema.

Amesema Korosho Queens imeanza mzunguko huo kwa ushindi wa seti 3-1 dhidi ya JKT, kabla ya kuifunga Genesis ya Kilimanjaro kwa seti 3-0 katika mchezo wa pili na mchezo mwingine walishinda dhidi ya Mafinga Parish seti 3-0 juzi.

Kibombwe amesema ushindi dhidi ya JKT ulikuwa muhimu kutokana na uzoefu wa wapinzani hao ambao wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na kufanya mazoezi kwa pamoja.

Akizungumzia ushindi dhidi ya Genesis, amesema wapinzani wao walikuwa wamejiandaa vizuri na walitoa upinzani mkubwa, lakini Korosho Queens ilikuwa bora zaidi kimbinu.

Ameongeza kuwa idadi ndogo ya wachezaji wa Genesis iliwapa nafasi ya kutumia vizuri mabadiliko ya wachezaji kulingana na mwenendo wa mchezo na hatimaye kupata ushindi.

Amesema malengo yao ni kuendelea kufanya vizuri hadi kufuzu hatua ya mchujo (playoff) na baadaye kucheza fainali, huku akimshukuru mdhamini wao, Bodi ya Korosho Tanzania, kwa kuwawezesha kujiandaa vizuri.

Kibombwe amesema benchi la ufundi limekuwa likifuatilia michezo ya wapinzani wao ili kujiandaa vizuri kabla ya kukutana nao, akiamini maandalizi hayo yatawasaidia kupata matokeo mazuri.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button