JWTZ, NM-AIST kukuza teknolojia za ndani ulinzi

ARUSHA: JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepanga kuingia makubaliano ya ushirikiano na Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia (NM-AIST), kwa lengo la kuendeleza tafiti na teknolojia za ndani zitakazosaidia kutatua changamoto za ulinzi na usalama nchini.

Mpango huo unalenga kutumia utaalamu wa watafiti na wataalamu wa ndani katika maeneo ya akili unde (AI), sayansi ya data na teknolojia nyingine, ili kuongeza uwezo wa Tanzania kubuni na kuzalisha teknolojia zake badala ya kutegemea suluhisho kutoka nje ya nchi.

Hayo yalisemwa jijini Arusha na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, wakati wa ziara yake katika NM-AIST, ambapo alitembelea na kujionea shughuli mbalimbali za utafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia zinazofanywa na taasisi hiyo.

Jenerali Mkunda alisema JWTZ limekuwa likitafuta teknolojia na utaalamu nje ya Tanzania, ikiwemo katika nchi mbalimbali barani Afrika, lakini ziara hiyo imeonesha kuwa kuna fursa ya kutumia uwezo na utaalamu uliopo ndani ya nchi.

Alisema ziara hiyo imelenga kufahamu kwa karibu uwezo wa NM-AIST na kubaini maeneo ambayo JWTZ linaweza kushirikiana na watafiti na wataalamu wa taasisi hiyo katika kutengeneza na kuendeleza teknolojia zitakazokidhi mahitaji ya nchi.

“Tumegundua kwamba tunakwenda nje ya Tanzania, mpaka Bara la Afrika, kwa ajili ya kutafuta teknolojia, kumbe tuna chuo ambacho tunaweza kupata teknolojia na kushirikiana kufanya tafiti mbalimbali hapa hapa nchini kwetu Tanzania,” alisema.

Jenerali Mkunda alisema hatua inayofuata ni kuandaa na kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) utakaoweka msingi wa ushirikiano rasmi kati ya JWTZ na NM-AIST katika tafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia.

Alisema ameridhishwa na ziara hiyo, akieleza kuwa imefungua fursa mpya ya kuimarisha mahusiano kati ya JWTZ na NM-AIST, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, alisema ziara hiyo imetoa fursa kwa JWTZ kujionea uwezo wa taasisi hiyo katika utafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia.

Alisema maeneo yanayotarajiwa kuwa sehemu ya ushirikiano huo ni pamoja na akili unde, sayansi ya data na teknolojia nyingine, ambazo zinaweza kusaidia kujenga uwezo wa Tanzania wa kubuni na kuzalisha teknolojia ndani ya nchi.

Profesa Kipanyula alisema ushirikiano huo utaunganisha nguvu, utaalamu na miundombinu ya taasisi hizo mbili, hatua ambayo itasaidia kuanza kuzalisha teknolojia na bunifu zenye manufaa ya moja kwa moja kwa taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button