Kigoma yapaa usajili makundi maalum NeST

KIGOMA: MKOA wa Kigoma umefanikiwa kusajili makundi maalumu 1,359 katika Mfumo wa Manunuzi ya Umma (NeST), hatua inayoyawezesha makundi hayo kushiriki katika utekelezaji wa mpango wa manunuzi ya umma katika taasisi za Serikali.

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Kati na Magharibi, Mhandisi Suma Atupele, ametoa taarifa hiyo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, wakati wa mkesha wa Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma.

Atupele amesema hadi kufikia Septemba 7 mwaka huu, halmashauri za Mkoa wa Kigoma zimetoa zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 500 kwa makundi hayo.

Amesema makundi yaliyosajiliwa katika mfumo huo yanajumuisha vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, huku idadi hiyo ikiwa imevuka lengo la PPRA la kusajili makundi maalum 1,200, sawa na makundi 150 kwa kila halmashauri.

Kwa mujibu wa Atupele, mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa mpango wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025–2050 unaozingatia uchumi jumuishi, ambao unataka asilimia 30 ya manunuzi ya taasisi za Serikali kufanywa na makundi maalum yaliyosajiliwa katika mfumo wa NeST.

Kufuatia mafanikio hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amezipongeza halmashauri za Mkoa wa Kigoma kwa kufikia na kuvuka malengo ya usajili wa makundi maalum na kuzitaka kuhakikisha zinatoa tenda kwa makundi hayo kwa kuzingatia asilimia 30 ya bajeti zao za manunuzi.

Mwang’onda amesisitiza kuwa halmashauri zinapaswa kuzingatia utaratibu wa kutoa tenda zenye thamani isiyozidi Sh milioni 500 kwa makundi hayo maalum, akisema kwa sasa makundi mengi yaliyosajiliwa yameonyesha uwezo wa kutekeleza zabuni hizo.

Awali, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Azizi Nurfus, amesema jumla ya makundi maalum 165 yamesajiliwa katika halmashauri hiyo kupitia mfumo wa ununuzi wa kielektroniki (NeST).

Amesema kuanzia mwaka 2024/2025, makundi maalum matatu yalipata tenda katika halmashauri hiyo zenye thamani ya Sh milioni 108, huku vikundi viwili vikipata tenda nje ya halmashauri hiyo zenye thamani ya Sh milioni 253.6.

Aidha, amesema kikundi kimoja kimepata tenda mbili nje ya Mkoa wa Kigoma zenye thamani ya Sh milioni 74.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button