Ziara ya mawaziri yaonesha suluhisho Pawaga, Isimani

IRINGA: Ziara ya Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bashiru Ally Kakulwa, katika eneo la Pawaga, Jimbo la Isimani, imeelezwa kuwa na tija kwa wananchi baada ya kuwezesha serikali kuona kwa pamoja changamoto za kilimo, mifugo na maji na kuanza kuweka mikakati ya kuzitatua.
Mbunge wa Isimani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda, alisema ziara hiyo imekuwa muhimu kwa sababu imewaleta pamoja mawaziri hao na viongozi wa Serikali katika eneo ambalo wananchi wanakabiliwa na changamoto zinazohitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali.
Alisema uwepo wa viongozi hao umeongeza matumaini ya kupata ufumbuzi wa changamoto za wananchi, huku akieleza kuwa tayari serikali ya mkoa na wilaya imeanza kuchukua hatua, hasa katika kukabiliana na tatizo la maji kwa mifugo.
“Baada ya kupata malalamiko kuhusu ukosefu wa maji kwa mifugo, nilifika hapa wiki iliyopita kuona hali halisi na nikakuta tayari serikali ya mkoa na wilaya imeanza kuchukua hatua,” alisema.
Alisema tayari kisima kimoja kimechimbwa kwa gharama ya Sh milioni 18, huku changamoto iliyobaki ikiwa ni upatikanaji wa pampu na mfumo wa kusukuma maji hadi maeneo yanayohitajika.

Mtatifikolo alisema kutokana na kutokuwepo kwa umeme wa uhakika katika eneo hilo, wameamua kutumia mfumo wa sola kuendesha pampu, ambao unakadiriwa kugharimu Sh milioni tisa.
Alisema tayari amechangia Sh500,000 na Diwani wa eneo hilo Sh200,000, huku wafugaji wakihamasishwa kuchangia ili kukamilisha mfumo huo na kuhakikisha mifugo inapata maji.
“Tumeweka lengo ndani ya wiki mbili tuwe tumepata fedha hizo ili tuweze kutoa maji pale chini na mifugo yote ipate maji,” alisema.
Mbunge huyo alisema wafugaji wamekubaliana kuchangia kati ya Sh100,000 na Sh200,000 kwa kila boma, hatua ambayo imeonesha utayari wa wananchi kushiriki katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Alisema pamoja na hatua hiyo, bado kuna uhitaji wa visima vingine takribani 10 katika maeneo mbalimbali, hivyo akaiomba Serikali na wadau kuendelea kushirikiana katika kukamilisha miradi hiyo kwa awamu.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisema ziara hiyo imelenga kuanza utekelezaji wa ushirikiano wa vitendo kati ya sekta ya kilimo na mifugo, kwa kutambua kuwa sekta hizo zinategemeana katika uzalishaji na uchumi wa wananchi.
Chongolo alisema Serikali imeamua kuunganisha nguvu za wizara na taasisi mbalimbali katika maeneo ambayo changamoto zake haziwezi kutatuliwa na sekta moja pekee.
“Tukakubaliana tufanye uzinduzi wa shughuli hii ya msingi ya kufanya kwa pamoja ili kuyatafuta matokeo yenye tija kwa wananchi, tukianzia hapa Pawaga, Jimbo la Isimani, Wilaya ya Iringa Vijijini,” alisema.
Alisema kufika eneo hilo kumewawezesha viongozi kuona hali halisi na kubaini changamoto zinazowakabili wananchi na wafugaji, jambo litakalosaidia kupanga hatua za kuzitatua kwa ufanisi zaidi.
Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bashiru Ally Kakulwa, alisema utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha ushirikiano baina ya sekta mbalimbali ni muhimu katika kuongeza tija na kutatua changamoto za uzalishaji.
Alisema kilimo na mifugo vina uhusiano wa karibu, hivyo Serikali inapaswa kuunganisha nguvu katika kushughulikia changamoto kama upatikanaji wa maji na malisho, hususan wakati wa mabadiliko ya tabianchi na ukame.
“Tumekuja hapa kuungana kwa pamoja kutangaza ushirikiano katika sekta ya kilimo na mifugo kwani mahitaji katika sekta hizo ni makubwa sana kwasababu ni msingi wa usalama wa chakula na lishe ya wananchi,” alisema.
Kakulwa alisema ushirikiano huo unahusisha pia Wizara ya Maji, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi nyingine, kwa kuwa mafanikio ya uzalishaji yanategemea upatikanaji wa miundombinu, masoko na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo.
Alisema serikali pia itaendelea kuhakikisha wafugaji wanapata huduma na mifumo inayowawezesha kufanya biashara ya mifugo kwa kuzingatia vipimo sahihi vinavyotambuliwa kisheria.



