Wananchi, Barrick wajenga shule Longido

ARUSHA: KAMPUNI ya kimataifa ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Barrick Gold, kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Kiseriani, Kata ya Engikaret, Wilaya ya Longido, Mkoa wa Arusha, Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Steven Kiruswa na Serikali, imefanikisha ujenzi wa shule shikizi kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 230.
Akizungumza katika uzinduzi wa shule hiyo kijijini hapo, Meneja Mkazi wa Barrick (Country Manager) Tanzania, Melkiory Ngido, alisema uamuzi wa kampuni hiyo kutoa msaada huo ulifuatia maombi ya Dkt Kiruswa, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, pamoja na kampuni hiyo kujionea hali halisi ya changamoto zinazowakabili wanafunzi.
Alisema wanafunzi hao walikuwa wakitembea umbali wa kilomita 32 kwenda na kurudi shuleni, hali ambayo ilikuwa ikihatarisha usalama wao kutokana na uwepo wa wanyama wakali katika maeneo wanayopita.
Ngido aliwaahidi wananchi wa Kiseriani na Longido kwa ujumla kuwa Barrick Gold itaendelea kushirikiana nao katika kujenga miundombinu ya elimu, kutokana na wananchi hao kuonyesha nia ya dhati, ushirikiano na uadilifu mkubwa katika ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya mwalimu.

Alisema kampuni hiyo imechangia zaidi ya Sh milioni 180 kwa ajili ya ujenzi huo na fedha hizo zimetumika kama ilivyokusudiwa.
“Barrick Gold imeamua kujitoa zaidi Longido kuhakikisha elimu inasogezwa karibu na maeneo ya makazi ya watu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, ofisi na nyumba za walimu inajengwa kwa maslahi ya watoto wa jamii hiyo,” alisema Ngido.
Alisema elimu ni msingi wa maisha na kwamba uamuzi wa wananchi wa Kijiji cha Kiseriani, ambao wengi wao ni jamii ya wafugaji wa Kimasai, kujitolea na kujenga madarasa mawili na ofisi ya mwalimu ni hatua inayopaswa kuungwa mkono.
Alisema hatua hiyo inaonyesha kuwa jamii hiyo imeamua kujitoa na kuwajali wanafunzi pamoja na kuweka msisitizo katika elimu.
Naye, Dk Kiruswa aliishukuru Barrick Gold kwa uamuzi wa kuchangia ujenzi wa madarasa na ofisi ya mwalimu, akiahidi kuendelea kushirikiana na kampuni hiyo na wananchi katika kuboresha huduma za jamii.
Alisema uamuzi huo unapaswa kupongezwa na wananchi wote wa Longido, akisisitiza kuwa uadilifu ni jambo muhimu katika kuwashawishi wafadhili wengine kujitoa kusaidia miradi ya miundombinu ya elimu, maji na barabara.
Alisema uamuzi wa wananchi wa kuanza ujenzi wa madarasa mengine mawili kwa kusomba mawe, mchanga na kokoto ni wa busara, na kwamba ataunga mkono juhudi hizo kwa kutoa mifuko 100 ya saruji pamoja na kugharamia upauaji.
Dk Kiruswa aliwaomba wananchi wa Kiseriani na Longido kwa ujumla kujitoa katika shughuli za kijamii, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya elimu, akiahidi kuwa atakuwa mstari wa mbele katika kuchangia na kutafuta wafadhili zaidi.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Longido, Papa Nakuta, amempongeza Dk Kiruswa kwa jinsi anavyojitoa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Longido.
Aliwataka wananchi kumuunga mkono mbunge huyo akisema amekwenda Bungeni kufanya kazi na si kulala, huku akieleza kuwa katika kila mradi unaotekelezwa jimboni humo, mchango wake upo, ama kwa yeye mwenyewe au kwa kuwaleta marafiki zake na kufanya ushawishi kwa Serikali kuendelea kupeleka fedha za miradi katika jimbo hilo.



