Kampuni 30 za Ujerumani kusaka fursa Tanzania

DAR ES SALAAM: Tanzania imepokea ujumbe wa wafanyabiashara na wakurugenzi wa kampuni 30 kutoka Ujerumani, walioambatana na Waziri wa Ujerumani, Manfred Pence, kwa lengo la kutafuta na kutathmini fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Ujerumani, ikiwa ni mwendelezo wa mkutano wa Invest East Africa Forum uliofanyika Januari mwaka huu nchini Ujerumani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema ujio wa ujumbe huo ni fursa muhimu kwa Tanzania kuongeza uwekezaji na kupanua wigo wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Kapinga amemshukuru Waziri Pence kwa kutenga muda wake na kuja Tanzania akiwa ameambatana na wakurugenzi wa kampuni hizo 30 kwa ajili ya kujionea fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Amesema kabla ya kukutana na wafanyabiashara hao, alifanya mazungumzo na Waziri Pence kuhusu maeneo mbalimbali ambayo Tanzania inaona yanaweza kuimarisha zaidi ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo.

“Kwa miaka saba iliyopita, ukiangalia ujazo wa biashara kati ya nchi zetu mbili, umeongezeka kwa takriban asilimia 96, huku thamani ya mauzo ya nje ikiongezeka kwa takriban asilimia 62,” amesema.

Hata hivyo, Kapinga alisema Tanzania bado ina nafasi kubwa ya kutumia fursa zilizopo kuongeza mauzo yake katika soko la Ujerumani na kuboresha zaidi urari wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Amesema Tanzania imebadilisha mwelekeo wa uwekezaji kwa kuweka mkazo katika uendelezaji wa viwanda na kuongeza thamani ya mazao badala ya kusafirisha malighafi nje ya nchi.

“Tumewaeleza namna ambavyo tunatamani michakato ya uwekezaji ijikite kwenye uendelezaji wa viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa, si kusafirisha malighafi nje,” amesema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mazungumzo hayo yalihusisha sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, madini, viwanda, dawa za binadamu, utalii na maeneo mengine yenye fursa za uwekezaji.

Amesema Tanzania tayari ina wawekezaji kutoka Ujerumani wanaofanya shughuli mbalimbali nchini, akitaja viwanda vya Kenaf na Tanga Cement kama baadhi ya mifano ya uwekezaji huo.

Kapinga amesema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji zaidi, kuongeza mitaji na kupanua shughuli zao nchini.

Kwa upande wake, Waziri Pence amesema ziara hiyo imeonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, akisisitiza kuwa ushirikiano huo si jambo la anasa bali ni msingi wa mafanikio kwa pande zote.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa Tanzania, Hessen, Afrika Mashariki na Ujerumani, akieleza kuwa Afrika ni bara lenye fursa nyingi za kiuchumi.

“Afrika ni bara lenye fursa nyingi na tunataka kuwa washirika wazuri katika kuzitumia fursa hizo,” amesema.

Ziara hiyo inatarajiwa kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kutoka Ujerumani kujionea mazingira ya uwekezaji nchini na kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano wa kibiashara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button