Ushauri wa JKT kwa vijana kuhusu matumizi ya mitandao

KIGOMA: Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele amewahimiza vijana wa Kitanzania kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na kuwasilisha ujumbe wenye manufaa kwa jamii na taifa.
Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa Mujibu wa Sheria kupitia “Operesheni Linda Amani” na vijana wa Kujitolea kupitia “Operesheni Nishati Safi”, yaliyofanyika katika Kikosi cha Kanembwa JKT mkoani Kigoma.
Amesema somo la uzalendo na uzalendo wa kidijitali katika silabasi za mafunzo ya JKT litaendelea kupewa kipaumbele na kuboreshwa, kwa lengo la kuwaelimisha vijana kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

Meja Jenerali Mabele amesema vijana wanapaswa kuepuka kurekodi na kusambaza maudhui yasiyofaa, ikiwemo matusi na ujumbe unaoweza kuleta migawanyiko katika jamii. Badala yake, amewataka kutumia mitandao hiyo kutangaza biashara, kutoa elimu na kusambaza ujumbe wenye tija kwa taifa.
SOMA: JKT mambo safi matumizi nishati safi
Katika hatua nyingine, ameiishukuru Serikali kwa kuendelea kuliwezesha JKT kuboresha miundombinu katika vikosi vyake ili kuongeza uwezo wa kutoa mafunzo kwa vijana wengi zaidi.
Mafunzo hayo yalianza Septemba 8, 2026 na yamekuwa ya kwanza kwa vijana wa Kundi la Lazima (Mujibu wa Sheria) Operesheni Linda Amani na Kundi la Kujitolea Operesheni Nishati Safi kuhitimisha mafunzo yao kwa pamoja.



