Miss Kanda ya Mashariki waanzisha mwendo

PWANI: Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nassir Ali, amesema serikali itaendelea kuunga mkono mashindano ya Miss Tanzania kwa kuwa yanaendana na jitihada za kukuza sanaa na kuweka mazingira ya vijana kutumia vipaji vyao kupata fursa za kiuchumi.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa Miss Tanzania Kanda ya Mashariki uliofanyika Kisemvule, Mkuranga mkoani Pwani Khadija amesema shindano hilo linahitaji kuungwa mkono na wadau na kampuni mbalimbali kuwasaidia wasichana kutimiza ndoto zao.
Amewataka wawekezaji na kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini Miss Kanda ya Mashariki akisema ushirikiano wa sekta binafsi utasaidia kufanikisha shindano hilo ambapo fainali yake itakuwa Oktoba 10, mwaka huu.
“Mkuranga ni historia kwetu kuasisi jambo hili kubwa, ambalo linaenda sambamba na sera ya serikali katika kuhakikisha tunaendelea kukuza sanaa na kuweka mazingira wezeshi kwa sanaa za aina zote kuibua ajira mbalimbali kwa vijana wetu, ili kufanikisha wadau wasapoti,” amesema.

Naye Yusuf Hassan, Mkurugenzi wa Miss Tanzania Kanda ya Mashariki, amesema mashindano hayo yatahusisha warembo kutoka Morogoro, Lindi, Mtwara na Pwani, huku warembo 16 watakaofaulu usaili wakitarajiwa kuingia kambini kuanzia Oktoba Mosi kwa ajili ya mafunzo mbalimbali.
Yusuf amesema bado wanahitaji wadhamini zaidi kwa kuwa bajeti ya mashindano hayo inakadiriwa kufikia takribani Sh milioni 210, hivyo kuomba kampuni na taasisi kujitokeza kuunga mkono.

Kwa upande wake, Aidan Rico, mwakilishi wa Kamati ya Miss Tanzania iliyo chini ya Lamata Village Entertainment Company Limited, Miss Kanda ya Mashariki imekuwa kanda ya kwanza kuzindua mashindano yake na kuwashukuru waandaaji pamoja na wadhamini waliojitokeza, huku akitoa wito kwa wadau wengine na serikali kuendelea kuunga mkono tasnia ya urembo.



