CCM yataka uwajibikaji miradi Temeke

DAR ES SALAAM: Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM ambaye pia ni Mlezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kenani Kihongosi, ameitaka TARURA na uongozi wa Wilaya ya Temeke kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi Group Six International Limited, kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake katika ujenzi wa barabara.

Kihongosi ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Masaki, akieleza kuwa Temeke imepatiwa miradi ya barabara yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 92, inayohusisha zaidi ya kilomita 55, ambapo kilomita 32 ziko katika hatua za ujenzi.
Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Temeke, Mhandisi Janeth Mwandiga, amesema mkandarasi huyo anasimamia ujenzi wa barabara za Masuliza yenye urefu wa kilomita 4.04 na Kilimahewa kilomita 7.382, kwa gharama ya Sh bilioni 25.9.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Mbagala, Kakulu Burchard, amesema ujenzi wa hospitali ya ghorofa saba yenye thamani ya Sh bilioni 17.7 unaendelea, huku ukitarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, ikiwemo matibabu ya kibingwa.
Naye, Mbunge wa Temeke, Mariam Kisanga, amesema Serikali inaendelea kujenga shule za msingi na sekondari, ikiwemo majengo ya ghorofa, kwa lengo la kuboresha mazingira ya elimu.

Akihitimisha ziara yake kwa mkutano wa hadhara Masuliza, Tuangoma, Kihongosi amewataka wananchi kudumisha amani na mshikamano, akisisitiza umuhimu wa utulivu katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.



