Serikali yamaliza mgogoro wa ardhi Bonde la Usangu

SERIKALI imeumaliza mgogoro wa matumizi ya ardhi wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya uliodumu kwa miaka 15, kati ya wakazi wa wilaya hiyo katika eneo la Bonde la Usangu dhidi ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imefanya maboresho kwenye Tangazo la Serikali Namba 28 ambayo itawawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu.
Majaliwa alisema hayo jijini Mbeya alipozungumza katika kikao na wadau waliowekeza katika Bonde la Usangu wakiwamo wakulima wa mashamba ya mpunga, mashine za kukoboa mpunga na wafugaji katika vitalu.
Alisema marekebisho ya tangazo hilo yatawezesha baadhi ya vitongoji vilivyokuwa vimetangazwa awali kuwa ndani ya hifadhi kuachwa nje ya mipaka ikiwamo kutoa eneo la hekta 74,000 kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

“Hii GN 28 serikali tumeamua kuitafutia ufumbuzi baada ya vikao vingi na wadau kwa faraja kabisa nataka niwaambie tumefikia hatua nzuri itakayowezesha kila anayejishughulisha na kilimo kuendelea na kilimo chake na kila anayejishughulisha na mifugo kuendelea na ufugaji wake,” alisema Majaliwa.
Alisema serikali inataka kuhakikisha Wilaya ya Mbarali inaendesha shughuli za kilimo kitaalamu na kwa tija.
“Tumeona maendeleo makubwa na ujenzi wa viwanda vya mtu mmoja mmoja na vikundi, serikali inataka kuona shughuli hizo zinakuwa endelevu, tunataka mpanue viwanda vyenu na mzalishe zaidi,” alisema Majaliwa.
Pia alisema serikali imeamua kuitoa nje ya hifadhi Ranchi ya Usangu kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa kisasa.
“GN namba 28 iliingiza ranchi ndani ya hifadhi, lakini ili wafugaji wawe huru tumeiondoa na hivyo itakuwa nje, tumeacha na mito kadhaa ambayo itahifadhiwa kwa sheria za mazingira,” alisema Majaliwa na kuwataka wafugaji wajiamini kwa kuwa mifugo ni uchumi.
“Tunataka tuondokane na uchungaji na kuwafanya Watanzania wafugaji kuacha kutembea umbali mrefu na ng’ombe kwani inaondoa thamani ya nyama, tunataka mfuge kisasa,” alifafanua.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema Ranchi ya Usangu ni kwa ajili ya shughuli za ufugaji tu.
“Tulioko kwenye ranchi tufuge, wengine mnabadilisha matumizi wengine hamfugi, lakini mnakodisha watu wanakuja kulima kwenye vitalu, wale mnaolima badala ya kufuga tutawanyang’anya vitalu,” alisema Ndaki.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula alisema maeneo yaliyoondolewa katika hifadhi yatawekewa mpango bora wa matumizi ya ardhi na wananchi watapata hati miliki za maeneo yao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo alisema kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji watumiaji wanapaswa kuheshimu sheria ya mazingira.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana aliwataka watumiaji wa eneo lililotolewa kwa shughuli za ufugaji na kilimo waendelee kulilinda eneo lililobaki.
“Tusifuge wala kulima katika eneo lililobaki eneo hili ni chanzo kikubwa cha maji na sehemu ya utalii,” alisema Dk Chana.



