Dk Bashiru atoa maagizo vyama vya ushirika

KAGERA: Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Bashiru Kwakurwa, amevitaka vyama vya ushirika kushirikiana na wakulima wao kutafuta taasisi za kifedha kwa ajili ya kupata elimu ya mikopo ili kuendeleza sekta ya kilimo, kuongeza thamani na ubora wa mazao pamoja na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi yanayozingatia ubora.

Akizungumza wakati wa kuzindua na kufungua tawi la Benki ya Ushirika (COOPBANK) katika Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Dk. Kwakurwa alisema benki hiyo imejikita katika kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupitia vyama vyao vya ushirika ili kuinua uchumi wao na kuongeza uzalishaji wenye tija na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Alisema benki hiyo inapaswa pia kuhakikisha wavuvi na wafugaji wanapata fursa sawa za kifedha, hususan katika kuongeza thamani ya bidhaa za maziwa, ngozi na nyama, pamoja na kuwawezesha wananchi wanaoanzisha vizimba vya ufugaji wa samaki, ambavyo vimekuwa na mchango katika kuongeza tija katika sekta ya uvuvi.

Kupitia ufunguzi wa tawi hilo, Waziri Kwakurwa aliwataka wafanyabiashara wanaojihusisha na mazao yatokanayo na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kubadilisha mtazamo wa kufanya biashara kwa kuongeza uzalishaji na kuwekeza katika shughuli zenye tija, akisema uwepo wa umeme wa uhakika utasaidia uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kushirikiana na wadau binafsi wanaolenga kuweka mazingira rafiki kwa wakopaji, huku akiitaka COOPBANK kuongeza uwajibikaji, uaminifu na uzalendo, pamoja na kuimarisha mifumo yake ili kuhakikisha huduma zake zinawanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.

Aidha, aliitaka benki hiyo kuongeza matawi katika mikoa mbalimbali nchini ili kutoa fursa sawa kwa wananchi kupata huduma za kifedha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa COOPBANK, Godfrey Ng’urah, alisema benki hiyo ilifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, mwezi Aprili 2025, na tawi lililofunguliwa Kagera ni la saba.

Alisema benki hiyo ina mpango wa kufikisha matawi 26 katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ifikapo mwaka 2030.

Ng’urah alisema Tanzania ina zaidi ya vyama 6,000 vya ushirika, hivyo benki hiyo inalenga kutumia mfumo wa kidijitali kuwafikishia huduma wananchi wanaojihusisha na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ikiwa na lengo la kuwafikia Watanzania milioni 10 ifikapo mwaka 2030.

Alisema tangu kuanzishwa kwake, benki hiyo imewezesha vyama vya ushirika vya kilimo na mifugo kupata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 66, huku Sh bilioni 6 zikitolewa katika sekta ya uvuvi kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuanzisha vizimba vya ufugaji wa samaki.

Alisema maono ya COOPBANK ni kujenga uchumi jumuishi, huku moja ya malengo yake makuu ikiwa ni kumtambua na kumuinua mkulima mdogo, mfugaji mdogo na wananchi wa vijijini, hususan wale wanaoishi maeneo ya pembezoni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa fursa za huduma za kifedha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa (KCU), Respikius Mashulano, aliiomba COOPBANK kufanya biashara kwa kuzingatia ushindani uliopo katika sekta ya fedha, pamoja na kuimarisha mifumo na huduma zake.

Mashulano alisema kuanguka kwa baadhi ya benki kumechangiwa na kutowajibika, ukosefu wa uadilifu, kutokuwa wabunifu na kushindwa kutambua ushindani uliopo katika biashara ya huduma za kifedha.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Ramadhani Kido, ameipongeza COOPBANK kwa kuanzisha huduma zake mkoani humo, huku akiomba wananchi wapewe elimu zaidi kuhusu umuhimu wa kutumia huduma za benki, elimu ya mikopo pamoja na umuhimu wa kujiunga na vyama vya ushirika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button