Dk Kida atoa wito ubunifu na teknolojia Dira 2050

DAR ES SALAAM; KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Tausi Kida amewataka wavumbuzi, watafiti, wajasiriamali na wadau wa maendeleo kuchunguza namna mawazo mapya, teknolojia, utafiti, ujasiriamali, fedha na ushirikiano wa kimkakati vinavyoweza kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ili kuharakisha maendeleo jumuishi na endelevu.
Akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Ubunifu Tanzania 2026 juzi Dar es Salaam, Dk Kida alisema wiki hiyo inaashiria mwanzo wa uhamasishaji wa kitaifa wa wavumbuzi, wajasiriamali, watunga sera, wawekezaji, watafiti, washirika wa maendeleo, watendaji wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Dira 2050.
Pia alisema wiki hiyo itafanyika kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 4, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, chini ya kaulimbiu isemayo ‘Kutoka Matarajio hadi Mabadiliko, Kubuni Njia ya Tanzania kuelekea Ustawi Jumuishi,’.
Alisema wiki hiyo inaonyesha hitaji la kusonga mbele zaidi ya matarajio kuelekea suluhisho za vitendo, ushirikiano na uwekezaji unaoweza kutafsiri uvumbuzi kuwa maboresho yanayopimika katika tija, ajira, ushindani, utoaji wa huduma za umma na ubora wa maisha.
Dk Kida alisema katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, mfumo wa ikolojia ya uvumbuzi nchini umekua kwa kiasi kikubwa, ukichangiwa na shughuli zinazokua kwa kasi katika maeneo ya ujasiriamali, teknolojia za kidijitali, utafiti na maendeleo, uvumbuzi wa kifedha, biashara zinazoongozwa na vijana pamoja na ushirikiano kati ya taasisi za umma na binafsi.
Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania, Shigeki Komatsubara alisema jukwaa hilo linaunganisha taasisi za serikali, washirika wa maendeleo, mashirika ya Umoja wa Mataifa, wasomi, taasisi za utafiti, taasisi za fedha, wawekezaji, viongozi wa sekta binafsi, wavumbuzi, wajasiriamali, mashirika ya vijana, asasi za kiraia na wataalamu wa teknolojia.
Alisema wadau hao watapata fursa ya kubadilishana maarifa, kutafuta suluhisho, kujenga ushirikiano na kuchangia ajenda ya uvumbuzi nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa Programu ya Funguo UNDP, Joseph Manirakiza alisema Wiki ya Ubunifu mwaka huu itatumika kama jukwaa shirikishi la kubadilisha mawazo ya washiriki kuwa nyenzo za ushirikiano, uwekezaji na suluhisho za vitendo katika kukuza maendeleo ya nchi.
Alisema programu hiyo pia itatoa nafasi kwa mazungumzo na ubadilishanaji wa maarifa, maonyesho ya uvumbuzi, majadiliano ya kimkakati, mitandao na ushirikiano miongoni mwa watendaji kutoka maeneo mbalimbali ya mfumo wa ikolojia ya uvumbuzi Tanzania.
Aliongeza kuwa washiriki watapata fursa ya kuchangia maarifa, suluhisho na kushiriki katika majadiliano yanayohusiana na maeneo ambayo ni vipaumbele vya maendeleo nchini Tanzania.



