Dk Kijaji akagua ujenzi wa soko Muleba

KAGERA: Waziri wa Maliasili na Utalii ameendelea na ziara katika Wilaya ya Muleba ambapo ametembelea mradi wa ujenzi wa soko kubwa la kisasa katika mji wa Muleba.
Akiwa Muleba, Dk Kijaji, amewataka wananchi kutunza amani ili waweze kunufaika na matunda ya uwekezaji wa serikali na kudai kuwa ikiwa wananchi hawatjivunia amani yao basi hawataweza kunufaika katika uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.

Aidha, aliwatakawananchi kuhakikisha wanakuwa wa kwanza kulinda miundombinu iliyowekwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kunufaisha vizazi vingi
Amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Muleba kwa ubunifu mkubwa wa ujenzi wa soko la kisasa ambalo litapunguza adha kwa wafanyabiashara wengi ambao wanakosa maeneo mazuri ya kufanyia biashara.

Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Ofisa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Dickson Mnyaga, amesema ujenzi wa soko hilo unagharimu zaidi ya Sh bilioni 4 katika awamu mbili.
Amesema awamu ya kwanza yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 2 imekamilika kwa asilimia 100, huku zaidi ya Sh bilioni 1 zikiwa tayari zimetumika. Aidha, awamu ya pili itagharimu zaidi ya Sh bilioni 1 na inatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Amesema hatua zilizosalia mpaka sasa ni uunganishaji wa umeme na uwekaji wa majina kwenye vyumba vya biashara.
Ametaja changamoto zinazoomjitokeza katika mradi huo kuwa ni ucheleweshaji wa upatikanaji wa baadhi ya vifaa vya ujenzi ambavyo havipatikani kwa urahisi ndani ya Mkoa wa Kagera, hali inayochangia kuchelewa kwa kukamilika kwa baadhi ya kazi kwa wakati.
Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan ujenzi wa Soko la Muleba, wakieleza kuwa mradi huo utakuwa chachu ya kukuza uchumi, kuongeza fursa za biashara na kuboresha maisha ya wananchi.



