Fadlu: Tunapaswa kusimama na Chasambi

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amemkingia kifua nyota wake, Ladack Chasambi kwa kusema anatakiwa kusaidiwa na sio kulaumiwa, kwa kosa la kujifunga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Fountain Gate Februari 6.

Simba imelazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo huo ikiwa ugenini uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati licha ya kuanza kupata bao la uongozi dakika 57 lakini dakika ya 75 Chasambi akajifunga baada ya kurudisha mpira kwa kipa wake, Moussa Camara.

Fadlu amesema ulikuwa mchezo mzuri, wa kiufundi na mbinu, lakini haikuwa siku yao na bao la kujifunga la Chasambi hatakiwi kulaumiwa bali kusaidiwa ili ajifunze zaidi kupitia makosa hayo.

Advertisement

“Chasambi ni kijana mdogo anatakiwa kulindwa kwa ajili ya kukilinda kipaji chake, bado anahitaji kusimamiwa na kupewa moyo kwa sababu ni hazina ya Taifa na hatakiwi kupotezwa,” amesema.

Fadlu amesema wanaendelea kuzungumza na nyota huyo kuendelea kumjenga na kumtengeneza kisaikolojia kwa ajili ya michezo ijayo ikiwemo dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa uwanja wa KMC, Mwenge Februari 11.

Kikosi cha Simba kinarejea jijini Dar es Salaam baada ya kuvuna alama nne kwenye michezo miwili ya ugenini kikiibuka na ushindi wa bao 3 -0 dhidi ya Tabora United kwenye uwanja wa Al Hassan Mwinyi kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Fountain Gate.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *