Helios Towers yaipiga ‘jeki’ maabara shule ya umma Bukoba

BUKOBA, KAGERA: Kampuni ya Helios Towers imezindua rasmi maabara ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Shule ya Sekondari Katale iliyopo wilaya Bukoba mkoani Kagera, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kurudisha fadhila kwa jamii kupitia uwekezaji katika sekta ya elimu na maendeleo ya kidijitali nchini Tanzania.
Mradi huo umefadhiliwa na Helios Towers Tanzania na kutekelezwa na Camara Education Tanzania, kwa ushirikiano wa karibu na uongozi wa shule pamoja na mamlaka za elimu za Wilaya ya Bukoba.

Mradi huu ambao umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 30, umewezesha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kisasa, ikiwemo kompyuta za mezani 25, kifaa cha kuonyesha picha (projector), televisheni ya kidijitali (Smart TV), ubao mweupe (whiteboard) pamoja na vifaa vya matengenezo ya TEHAMA (maintenance kit).
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa masoko na mauzo kutoka Helios, Ellen Lupilli, amesema maabara hiyo itawasaidia wanafunzi katika kujifunza masomo ya TEHAMA na lengo lao ni kufikia shuke nyingi hata za vijijini.

Kwa upande wake Dayani Mbowe ambaye ni Mkurugenzi wa Camara Education Tanzania amesema uzinduzi huo ni mwanzo lakini mpango wao ni kufikisha TEHEMA kila shule kama Serikali ambavyo imekuwa ikihimiza somo hilo ili kuendana na dunia ya kidigitali.
Akimwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Consolata Joseph amesema vifaa hivi vitarahisha ufundishaji wa TEHAMA, hatua inayotoa msukumo kwa wanafunzi kusoma masomo hayo yanayoendana na ulimwengu wa teknolojia.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu katika kuunga juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali kuhakikisha TEHAMA inakuwa kuendana na dunia ya sasa.
Naye mkuu wa Shule ya Sekondari Katale, Basharu Hussein pamoja na wanafunzi wa shule hiyo, wameishukru Helios Towers kwa vifaa hivyo, huku wakiahidi kuvitumia kikamilifu katika masomo yao.



