‘Huduma upimaji bidhaa kuendelea kuimarishwa’

MWANZA; Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za upimaji nchini, huku ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa mengine pamoja na kutoa fursa kwa nchi hizo kutumia miundombinu iliyopo na Tanzania kunufaika na uwekezaji huo.
Amesema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea ujenzi wa Jengo la Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jijini Mwanza, Septemba 9, 2026, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi na usalama wa miundombinu kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika ununuzi wa vifaa vya kisasa.
Aidha Londo amemtaka mkandarasi wa jengo hilo kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa wakati, kwani kukamilika kwa jengo hilo litakalokuwa na ofisi pamoja na maabara mbalimbali litarahisisha utoaji wa huduma za maabara na utawala kwa wafanyabiashara wa kanda ya ziwa.

Pia amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kuhakikisha utekelezaji wa miradi na uwekezaji unaofanyika katika miundombinu unawanufaisha wananchi wa maeneo husika, ikiwemo kupitia upatikanaji wa huduma bora, kuongezeka kwa fursa za kiuchumi na kuwezesha wafanyabiashara kupata huduma kwa urahisi na kwa wakati.
Amesema ni vema TBS kutumia fursa zilizopo kushawishi jumuiya za kimataifa kuwekeza katika vifaa vya vipimo na teknolojia za kisasa katika maabara zilizopo nchini, ili kuongeza uwezo wa maabara hizo kutoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Amesema ushirikiano huo utasaidia Tanzania kuendelea kujenga uwezo katika eneo la upimaji, kuvutia matumizi ya huduma za maabara kutoka nchi nyingine na kuongeza fursa za uwekezaji, huku ukichangia katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha huduma za upimaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.



