Kagera: Mwenge wa Uhuru kuzindua miradi ya bil 23.7/-

KAGERA: Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 unatarajiwa kuzindua, kufungua, kutembelea kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 54 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 23.7 mkoani Kagera.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, amesema mwenge huo utapokelewa wilayani Muleba katika Kijiji cha Nyakabango ukitokea mkoani Geita Agosti 30, 2026, kabla ya kuanza kukimbizwa katika halmashauri nane za Mkoa wa Kagera.
Kwa mujibu wa Kanali Kido, Mwenge wa Uhuru utatembea umbali wa takribani kilomita 1,230 ndani ya Kagera, huku ukiifikia miradi 54 katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo,katika miradi hiyo, 25 itawekewa mawe ya msingi, mitano itafunguliwa, 11 itazinduliwa na 13 itakaguliwa ili kujiridhisha na utekelezaji wake pamoja na manufaa yake kwa wananchi.
Miradi hiyo inahusisha sekta muhimu za maendeleo, ikiwemo maji, afya, elimu, miundombinu, nishati, uwezeshaji wa vijana kiuchumi, pamoja na mazingira wezeshi kwa uwekezaji.
Alisema ujumbe mkuu wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu unalenga kuendelea kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, kupitia kaulimbiu:
“Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”



