KCJE yatajwa mfano wa usimamizi bora wa zao la korosho

MTWARA: Mradi wa Pamoja wa Vyama Vikuu vya Ushirika vya Pamba nchini (TANCCOOPS) umeipongeza Kamati ya Pamoja ya Vyama Vikuu vya Ushirika vya Korosho nchini (KCJE) kwa faida mbalimbali zinazopatikana kwa wakulima wa zao la korosho kupitia mradi huo, ikiwemo upatikanaji wa pembejeo kwa wakati.

Hayo yamejiri leo, Agosti 18, 2026, wakati wanachama wa TANCCOOPS walipotembelea mkoani Mtwara kwa lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya maendeleo yanayofanywa na KCJE kwa wakulima wa korosho.

Katika ziara hiyo, wanachama hao walijifunza kuhusu utoaji wa pembejeo za korosho, uimarishaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani unaompa mkulima uhakika wa kipato pamoja na masuala mengine yanayohusu maendeleo ya zao hilo.

Mwenyekiti wa TANCCOOPS, Leonard Nyabalima, amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kubadilishana uzoefu, hasa katika maeneo ambayo KCJE imepiga hatua na kufanya mabadiliko yanayowezesha sekta ya korosho kusonga mbele.

“Ni ziara ambayo tunaona kwetu ina tija na itatujengea uwezo wa kwenda kuyatekeleza yale tuliyoyaona ni mazuri kwa wenzetu, ambayo yana tija katika kusaidia sekta ya ushirika, hasa ushirika wa pamba hapa nchini,” amesema Leonard.

Mwanachama mwingine wa TANCCOOPS, Saidi Tangawizi, amesema wamejifunza namna KCJE inavyosimamia zao la korosho, hususan katika utoaji wa huduma kwa wakulima, ikiwemo upatikanaji wa pembejeo kwa wakati.

Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza, ameipongeza TANCCOOPS kwa kutembelea mkoa huo kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu teknolojia na namna ya kuendesha shughuli za ushirika.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa KCJE, Mohamed Nassoro, amesema ujio wa TANCCOOPS ni faraja kubwa kwao kwa kuwa unaonesha kuwa KCJE imeweza kutambulika, kujijengea uwezo na kuaminiwa na wadau mbalimbali wanaosimamia sekta tofauti na zao la korosho.

“Tumewapokea viongozi takribani ishirini na moja kutoka TANCCOOPS ambao wamekuja kujifunza namna KCJE imefanikiwa katika shughuli zake mbalimbali, ikiwemo usimamizi wa pembejeo, ambapo viongozi wamefurahi sana,” amesema Mohamed.

Amesema tangu Serikali ilipowapa dhamana ya kusimamia manunuzi ya pembejeo za zao la korosho, wameweza kununua pembejeo zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 840 na kuzisambaza katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema uzoefu huo umeendelea kuifanya KCJE kuwa sehemu muhimu katika kuhakikisha wakulima wa korosho wanapata huduma muhimu kwa wakati na kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button