Kituo cha afya Kiromba chapata gari mpya ya wagonjwa

MTWARA: SERIKALI imekabidhi gari kwenye Kituo cha Afya Kiromba kilichopo Kata ya Kiromba Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara litakayotumika kubeba wagonjwa kwenye maeneo hayo.

Zoezi la kukabidhi gari hilo limefanyika leo Septemba 11,2026 katika kijiji na kata ya kiromba wakati wa mkutano wa hadhara uliyofanyika kwenye kijiji hicho.

Mkutano huo umefanywa na Mbunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani humo, Abdallah Chikota kuhusu kuwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kuendelea kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 sambamba na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.

Kwa upande wake mbunge huyo amesema gari hiyo itumike katika matumizi sahihi yaliyopangwa na siyo kinyume na hapo.

“Hii gari ni kwa ajili ya kubeba wagonjwa, mfano Bp imeongezeka au mtu amedondoka anachuliwa kama itatakiwa kupelekwa ligula anapelekwa gari inarudi hapa”amesisitiza Chikota

Pia amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyolitupia jicho jimbo hilo kwani kati ya vituo vya afya vitano vilivyopo kwa sasa na hospitali ya halmashauri ya mji huo wamebakiwa kituo kimoja cha kitaya lakini vituo vyote vimeshapata magari ya kubeba wagonjwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Nassoro Jamali ametumia nafasi hiyo kuwaelekeza watumishi wote wa halmashauri kuwa gari hiyo ni ya umma hivyo inatakiwa ilindwe na kutunzwa.

“Endapo mwananchi atakuwa na changamoto ya kiafya atafika kituoni akaambiwa changia mafuta hilo suala serikali imezuia mgonjwa hatakiwi kuchangia huduma yeyote endapo atakuwa na dharula ya kutumia gari la wagonjwa”amesema Nassoro

Naye Diwani wa kata hiyo Hamisi Dadi ameishukuru serikali kwa kuendelea kuthamini uhai wa wananchi wakiwemo wa kata hiyo na kuridhia kuwapatia gari.

Baadhi ya wananchi wa kata hiyo akiwemo Anifa Salumu amesema uwepo wa huduma hiyo kutasaidia wananchi hao lakini kwa akina mama wakati wa kujifungua endapo mama mjamzito atakuwa na changamoto itayopelekea kuhamishiwa hospitali nyingine kama vile ya rufaa ya ligula na zingine.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button