Kliniki ya viwango ya TBS yavutia wengi Dar

DAR ES SALAAM; SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limeendelea kusogeza huduma na elimu kuhusu viwango, ubora na usalama wa bidhaa karibu na wananchi kupitia Kliniki ya Viwango, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo na kuwezesha wafanyabiashara kuzingatia matakwa ya viwango.

Akizungumza wakati wa Kliniki hiyo inayoendelea Kariakoo na Mwenge jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Yusuph, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ameipongeza TBS kwa kuendelea kuwafikishia wananchi huduma hizo, akisema zina mchango mkubwa katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa, kusambazwa na kuuzwa nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Yusuph amesema huduma zinazotolewa na TBS, ikiwemo upimaji, ukaguzi, usajili wa bidhaa na majengo pamoja na elimu kwa umma, ni muhimu katika kulinda afya za wananchi na kujenga imani katika bidhaa zinazouzwa sokoni.

Amesema usalama wa chakula na bidhaa si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja, huku akiwataka wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa wanazozalisha na kuuza ni salama na zinakidhi matakwa ya viwango.

“Bidhaa zenye ubora humjengea mfanyabiashara jina zuri, kuongeza imani kwa mlaji na kufungua fursa zaidi za biashara,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Habakuki Kalebo, amesema usalama wa vyakula na vipodozi ni wajibu wa wadau wote, hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuhakikisha bidhaa zao ni salama na zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Kalebo amesema kwa mujibu wa mwongozo wa TBS, wafanyabiashara wa chakula na vipodozi wanapaswa kusajili maeneo yao ya biashara, yakiwemo maduka, maghala, hoteli, migahawa na maeneo mengine yanayohusika na biashara ya vyakula na vipodozi.

Amewataka wafanyabiashara kutumia fursa ya Kliniki ya Viwango kupata elimu na huduma za usajili, akisisitiza kuwa viwango ni sehemu muhimu ya ulinzi wa afya za wananchi, bidhaa na uaminifu katika soko.

“Tunawashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma hii kwa karibu na elimu kuhusu mahitaji ya viwango,” amesema.

Ameongeza kuwa Kliniki ya Viwango imefanyika Kariakoo na Mwenge na itaendelea katika mikoa mbalimbali ambako TBS ina ofisi za kanda.

Kalebo amesema TBS inaendelea kushirikiana na halmashauri nchini katika kutoa huduma za usajili na ukaguzi wa maeneo ya biashara za vyakula na vipodozi, kuanzia ngazi za chini hadi taifa.

Akizungumza kama mmoja wa wanufaika wa Kliniki hiyo, mfanyabiashara Sajobe amesema huduma hiyo imewarahisishia wafanyabiashara kupata huduma za TBS bila kulazimika kwenda mbali.

Alisema awali wafanyabiashara walilazimika kufuata huduma hizo katika maeneo mengine, lakini uwepo wa kliniki Kariakoo umewarahisishia kushughulikia changamoto zao kwa haraka.

“Nimenufaika zaidi kwa sababu wamenirahisishia kusajili kwa haraka bidhaa zote ninazoagiza kutoka nje. Nimefanikiwa kusajili bidhaa nyingi kwa muda mfupi na zoezi limekuwa rahisi zaidi,” amesema.

 

Kliniki hiyo imekuwa pia fursa kwa wafanyabiashara kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu viwango, usajili na usalama wa bidhaa, huku TBS ikiendelea kusisitiza ushirikiano kati yake, wafanyabiashara, wananchi na mamlaka za Serikali katika kuhakikisha bidhaa zinazowafikia walaji ni salama na zenye ubora.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button