Mkwasa: Amani ni ushindi mkubwa kwa Watanzania

DAR ES SALAAM: NYOTA wa zamani wa Yanga ya Dar es Salaam na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ , Charles Mkwasa, amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya Tanzania na kwamba michezo, hususan soka, inapaswa kuendelea kuwa daraja la kuwaunganisha Watanzania badala ya kuwa chanzo cha migawanyiko.
Akizungumza na DailyNews Digital, Mkwasa amesema uzoefu wake wa miaka mingi ndani ya soka umemfundisha kuwa uwanjani hakuna tofauti za kisiasa, dini wala kabila, kwani mashabiki hukusanyika kwa lengo moja la kuisapoti timu yao na taifa lao.
Amesema licha ya Watanzania kuwa na mitazamo tofauti ya kisiasa, wanapokuwa viwanjani, tofauti hizo hutoweka na nafasi yake kuchukuliwa na mshikamano na uzalendo.
“Unaweza ukakuta mmoja ni wa CCM, mwingine ni wa CHADEMA, lakini wakifika uwanjani wote wanakuwa kitu kimoja. Wanasahau tofauti zao na wanaiunga mkono timu yao. Hiyo ndiyo nguvu ya michezo,” amesema Mkwasa ambaye pia amepata kuwa Kocha Mkuu wa Yanga na Taifa Stars.

Mkwasa ambaye amepata pia kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, amesema hali hiyo ndiyo inapaswa kuendelezwa hata nje ya viwanja, kwani taifa lenye amani huwapa wananchi nafasi ya kufanya kazi, kuwekeza na kufurahia maisha bila hofu.
Ameongeza kuwa katika safari zake za kimichezo ndani na nje ya Tanzania amejionea namna ambavyo nchi zenye utulivu zinavyofanikiwa kuandaa mashindano makubwa na kuvutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa Mkwasa, Watanzania wanapaswa kuendelea kulinda tunu ya amani waliyoachiwa na waasisi wa taifa, kwa kuwa bila amani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana.
“Nchi yetu imejengwa katika msingi wa amani. Hiyo ndiyo tunu kubwa tuliyonayo na kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda,” amesema ambaye wakati akisakata soka alipachikwa jina la Master..
Amewahimiza viongozi wa serikali, vyama vya siasa, taasisi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuendelea kuhubiri maridhiano na kuheshimiana hata wanapotofautiana kimtazamo.



