Mradi mpya kupunguza msongamano bandari ya Dar

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema eneo la Kurasi Logistics Park linatarajiwa kuanza kutumika kama sehemu ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam (Port Extension) kuanzia Novemba mwaka huu, hatua inayolenga kupunguza msongamano bandarini na kuongeza ufanisi wa huduma za mizigo.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya eneo hilo, Prof. Mbarawa amesema Serikali imekubaliana kulitumia eneo hilo si kama Kituo Kikuu cha Mizigo ya Nchi Kavu (ICD), bali kama sehemu ya bandari ambako shughuli za ukaguzi, uondoaji wa mizigo na huduma nyingine za Serikali zitafanyika.

Amesema matumizi ya eneo hilo kama Port Extension yatawezesha baadhi ya makontena kushushwa katika Bandari ya Dar es Salaam na kuhamishiwa Kurasi Logistics Park, ambako taratibu za ukaguzi na uondoshaji wa mizigo zitafanyika.
“Lengo kubwa ni kuhakikisha tunatumia eneo hili kama sehemu ya bandari ili kupunguza sana msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam. Mzigo utashukia pale bandarini, lakini clearance yote itafanyika hapa,” amesema Prof. Mbarawa.
Ameeleza kuwa ili mpango huo utekelezwe kwa ufanisi, Serikali imeweka masharti kadhaa, ikiwemo kuwepo kwa mobile scanners katika eneo hilo ili mizigo inayohamishiwa Kurasi ikaguliwe bila kulazimika kurudi bandarini.
Pia, amesema barabara inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kurasi Logistics Park itapaswa kutambuliwa kama Customs Bonded Road, ili kuwezesha usafirishaji salama wa mizigo kutoka bandarini hadi eneo hilo chini ya usimamizi wa mamlaka husika.

Prof. Mbarawa amesema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeelekezwa kushirikiana na TARURA, TANROADS na Halmashauri kuhakikisha barabara hiyo inakuwa maalumu kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda Kurasi.
“Mzigo ukitoka bandarini hautapita kwenye scanner pale. Utakuja kuscaniwa hapa. Ili kufanya hivyo, lazima barabara ile iwe Customs Bonded Road, TRA iweidhinishe na iwekwe mifumo ya ulinzi na ufuatiliaji,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Mbarawa, awali eneo hilo lilikuwa limekusudiwa zaidi kwa ajili ya kuhifadhia makontena, lakini Serikali sasa inalenga kulifanya kuwa sehemu ya shughuli za bandari ili kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo inayoongezeka.
Amesema kwa kuanzia, eneo hilo litatumika kuhudumia makontena ya mizigo inayoingia nchini (import containers), huku mpango wa kushughulikia mizigo ya nje (export containers) ukifuatia baada ya changamoto zilizopo kutatuliwa.
Prof. Mbarawa amesema endapo maandalizi yataenda kama yalivyopangwa, kufikia Novemba eneo hilo litakuwa limekamilika kwa matumizi kama Port Extension, huku TPA, TRA na taasisi nyingine za Serikali zitakazohusika na huduma za mizigo zikiwa na uwepo katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa hatua hiyo itasaidia wananchi kupata mizigo yao kwa haraka zaidi, huku ikipunguza msongamano wa magari na makontena katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi wa bandari hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Galus Abed, amesema kuongezeka kwa shughuli za bandari na ukuaji wa mji kumeongeza changamoto za msongamano wa malori na mizigo katika maeneo yanayozunguka bandari.
Amesema Serikali imeendelea kuweka miundombinu kama Kurasi Logistics Park ili kuwa na uwezo wa kuhifadhi malori na mizigo kabla ya kuondoka katika Bandari ya Dar es Salaam.
Abed amesema ongezeko la shughuli za bandari limekuwa kubwa, akieleza kuwa katika kipindi cha miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la takribani tani milioni sita za mizigo, hali ambayo imeongeza shinikizo kwenye miundombinu ya barabara.
Ameahidi kuwa mamlaka husika itatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mbarawa ili kuhakikisha eneo hilo linaanza kutoa huduma na kusaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam.



