Mwenge wa Uhuru watua Kagera

MULEBA: Mkoa wa Geita umekabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Kagera katika hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Nyakabango, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, huku viongozi mbalimbali na wananchi wakishiriki mapokezi hayo.
Mwenge huo umekabidhiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Steven Ndanki, katika hafla iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, amezitaka taasisi zote za manunuzi na Halmashauri nane za Mkoa wa Kagera kutenga asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi kwa ajili ya vikundi vilivyosajiliwa vya makundi maalum, wakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Amesema fedha hizo zinapaswa kuelekezwa katika vikundi hivyo ili viweze kukopeshwa na kuanzisha miradi ya maendeleo itakayowainua kiuchumi na kuwawezesha kujikwamua kutoka katika umaskini.

Aidha, amezitaka taasisi na mashirika ya umma kutoa kipaumbele kwa zabuni na tenda zisizozidi Sh milioni 500 ili ziweze kunufaisha makundi hayo, huku akizitaka Halmashauri zote nchini kusajili vikundi 150 kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata mikopo na kuanzisha miradi ya maendeleo.
Mwang’onda pia amewataka wananchi wa Mkoa wa Kagera kutumia mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 kama fursa ya kuchochea maendeleo, badala ya kuzigeuza kuwa chanzo cha migogoro.
Amesema endapo kuna changamoto kati ya wananchi na viongozi wao, zinapaswa kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi ili wananchi waendelee kusonga mbele katika kuleta maendeleo.

Akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Yahya Ramadhani Kido, amesema tayari mkoa umesajili vikundi 1,455 kati ya 1,200 vilivyohitajika, sawa na asilimia 121.
Amesema kati ya vikundi hivyo, vikundi 54 vimenufaika na fedha zilizotengwa kupitia mfumo wa manunuzi.
Kanali Kido amesema Mwenge wa Uhuru utatembea umbali wa takribani kilomita 1,230 ndani ya Mkoa wa Kagera na kutembelea miradi 54 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 23.7.

Amesema kati ya miradi hiyo, 25 itawekewa mawe ya msingi, mitano itafunguliwa, 11 itazinduliwa na 13 itakaguliwa ili kujiridhisha kuhusu utekelezaji wake pamoja na manufaa yake kwa wananchi.
Ameeleza kuwa miradi hiyo inahusisha sekta muhimu za maendeleo, zikiwemo maji, afya, elimu, miundombinu, nishati, uwezeshaji wa vijana kiuchumi pamoja na mazingira wezeshi kwa uwekezaji.
Kwa mujibu wa Kanali Kido, ujumbe mkuu wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu unalenga kuendelea kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia kaulimbiu isemayo: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”

Amesema Mwenge huo pia utatumika kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, malaria, VVU/UKIMWI na dawa za kulevya, sambamba na kuhimiza wananchi kuzingatia lishe bora.
Aidha, amewaalika wananchi wote wa Kagera kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru katika maeneo mbalimbali utakakopita, akisisitiza umuhimu wa kuonyesha mshikamano na kuunga mkono jitihada za maendeleo.



