Mzee Masabala atunukiwa tuzo mchango wa elimu Kibeta

KAGERA: Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, amemtunuku hati ya shukrani na tuzo Mzee Joseph Masabala, maarufu kama mzee mashuhuri wa Mkoa wa Kagera, kwa kutoa sehemu ya ardhi yake iliyopo Kata ya Kibeta, Manispaa ya Bukoba, kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kibeta.
Mzee Masabala na mkewe, Lushaka Masabala, wamepokea hati hiyo leo wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ulipofika katika shule hiyo na kuzindua vyumba viwili vya madarasa pamoja na kukabidhi madawati kwa wanafunzi.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mwang’onda ameipongeza familia ya Mzee Masabala kwa kufanya uamuzi wa pamoja wa kutoa ardhi hiyo na kulipa kipaumbele suala la elimu.
Amesema ardhi hiyo inaenda kuwa mkombozi wa elimu kwa kizazi cha sasa na kijacho, kutokana na mchango wake katika kuwezesha ujenzi wa miundombinu muhimu ya elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amesema ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi utaongeza ufaulu katika shule hiyo, sambamba na kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi.
Katika ziara yake Manispaa ya Bukoba, Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 umezindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 900.



